Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi wa msikiti wasitishwa Udom, Ponda alia na uongozi

41130 Pic+ponda Ujenzi wa msikiti wasitishwa Udom, Ponda alia na uongozi

Tue, 12 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amesema jumuiya imesikitishwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wa kusitisha ujenzi wa msikiti uliokuwa ujengwe chuoni hapo.

Akizungumza na wanahabari leo, Jumapili Februari 10, 2019 ofisini kwake Ilala, Sheikh Ponda amesema mwaka 2016 Waislamu waliomba eneo la kujenga msikiti na uongozi wa chuo hicho uliwakubalia kwa kuwapa ekari 10.

Ponda anasema mwaka huo huo, walianza kushughulikia vibali vya ujenzi katika mamlaka za chuo hicho na nje na walifanikiwa kuvipata vyote na  mwaka jana waliwasilisha nyaraka za ujenzi kwa menejimenti ya chuo na kisha kuingia mkataba na mkandarasi ambaye alianza kujenga kwa kuweka uzio wa mabati.

 

“Katika hali isiyotarajiwa Januari 9, 2019 uongozi wa Udom uliwaita viongozi wa Kiislamu na kuwaeleza amri ya kusitisha ujenzi huo. Waliwaeleza kuwa amri hiyo imetoka kwa mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka,” amedai Ponda.

Ponda amesema baada ya kikao hicho, baadaye uongozi wa chuo hicho ulichukua hatua ya kuvunja uzio wa msikiti huo chini ya usimamizi wa polisi na siku ya pili uliwakabidhi barua ya kuthibitisha uvunjaji huo.

“Jambo hili limetusikitisha sana, kwa sababu wahusika walifuata taratibu zote lakini ghafla wanaambiwa wasijenge na sababu ombi lao lilikubaliwa na uongozi uliopita na si wa sasa,”anasema Ponda.

Ponda amesema jumuiya hiyo imeazimia mambo mbalimbali ikiwemo kulaani tukio hilo, kuitaka Serikali iwabane waliohusika ili walipe gharama za ujenzi sanjari na kutoa tamko rasmi kuhusu hatua hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Kabaka amesema  kilichofanyika na watu hao ni kukiuka taratibu na hawakupewa kibali na mamlaka husika kujenga nyumba hiyo ya ibada.

“Kile kiwanja kipo ndani ya chuo na wao hawakuwa na idhini wala kibali cha ujenzi. Pia hakukuwa na bango lolote linaloonyesha kuwa kuna ujenzi na mkandarasi ni nani, ndio maana walikuwa wanapitisha malighafi zao usiku na polisi hawakutumika kuvunja uzio bali walinzi wa Suma- JKT,” amesema.

Kabaka amefafanua kuwa eneo hilo, liliachwa wazi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuabudu kwa dini zote mbili, lakini uongozi wa chuo ulikuwa bado haujatoa mwongozo wa ujenzi kwa kuwa walikuwa wakiendelea na vikao vya kujadili mchakato huo.

“Idhini ya ujenzi ikiwemo mali inayohamishika na isiyohamishika inatolewa na baraza la chuo na ndilo lenye mamlaka kamili. Tulipanga tukae tujadili kisha tutoe utaratibu na mwongozo kwa dini zote mbili msikiti ukae huku na kanisa kule, lakini wenzetu wametuwahi na kila mtu pale chuo ameshangazwa na hatua yao,” amesema.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz