Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uislamu unaamrisha kusoma kila elimu yenye manufaa

49410 Uislam+pic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Elimu ni kukijua kitu katika uhalisia wa vile kilivyo. Na ujinga ni kutokijua kitu katika uhalisia wa vile kilivyo.

Kwa muktadha huo, mwanadamu anaweza akawa ni mjuzi katika jambo fulani lakini akawa ni mjinga katika lingine. Na mwanaadamu kimaumbile hawezi kuwa na elimu ya vitu vyote.

Uislamu unapoamrisha kutafuta elimu, ni kwa sababu wanadamu wanaihitajia katika maisha yao na uhusiano wao na Mola. Uislamu haubagui elimu kwa kuwa inahitajika katika kutimiza uhusiano wa viumbe na Muumba wao na pia baina yao wenyewe.

Anasema Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam): “Si mbora wenu yule ambaye anaiacha dunia yake kwa sababu ya akhera yake na wala si mbora yule ambaye anaiacha akhera yake kwa sababu ya dunia yake mpaka akusanye vyote.”

Akaelekeza tena Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kwa kusema: “Fanya pupa ya dunia yako kama vile utaishi milele na fanya matendo ya akhera yako kama vile unakufa kesho.”

Mafunzo yote mawili hapo juu yanalenga mtu kutakiwa ashughulikie dunia yake na akhera yake kwa pamoja.

Ili yafikiwe malengo ya dunia na akhera, Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) anasema: “Yeyote mwenye kuitaka dunia na asome, na yeyote mwenye kuitaka akhera na asome, na mwenye kutaka zote (dunia na akhera) na asome.”

Hakuna kutenganisha elimu

Muislamu anatakiwa afahamu kwamba kujua elimu zote ili aweze kukidhi hitajio la maisha ya kimwili na kiroho ni wajibu. Hivyo basi dhana ya kuzitenganisha elimu (elimu ya dunia na elimu ya akhera) siyo dhana sahihi.

Mwanadamu ameumbwa katika mahitajio ya kimwili hivyo lazima elimu itakayotosha kukidhi mahitajio hayo iwepo.

Pia, mwanadamu analazimika kujua fika amri za Mola wake na makatazo yake ili azitekeleze ipasavyo.

Waislamu wanaodhania kwamba Uislamu hauhitajii elimu hizi za kimaisha (mazingira) wanatakiwa kubadili mtazamo huo kwa kuwa kitabu chetu kitukufu cha Quran katika Aya kadhaa kimezungumzia na kuelekeza mambo ya kidunia na dunia haitekelezeki bila ya elimu.

Katika Sura ya 28 (Al-Qasas) Aya ya 77, Mwenyezi Mungu anasema: “Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera, na wala usisahau fungu lako la dunia na wewe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema wewe na wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.”

Kwa kuwa Uislamu haubagui elimu ni vizuri jamii ikafahamu kwamba kwa ujumla Uislamu unalazimisha kusoma kila elimu, ambayo katika maisha inahitajika na kila elimu ambayo katika ibada inahitajika.

Jambo muhimu la kukumbushana ni kwamba tujirekebishe juu ya hii tabia ya kupuuza kusoma elimu ya dini, kwani msomi yeyote aliyesoma vyema dunia yake lakini hana chochote katika dini, huyo ni ‘mja hatarishi’ kwani anaweza kufanya lolote kwa sababu kinga ya mwanaadamu ni dini.

Pia, dini bila ya kuisomea huwezi kuitekeleza ipasavyo zaidi ya kufanya ushabiki ambao unaweza kubadilika wakati wowote.

Hata wale ambao wanawalipia watoto wao fedha nyingi ili wasome vizuri na wapate ajira nzuri, ni vyema wakatafakari na kujiuliza kwamba baada ya ajira nzuri mbele yao ni kifo na baada ya kifo ni kukutana na Mola Muumba.

Je, wamejiandaa? Je, wameandaliwa? Watamjibu nini Mola wao Muumba? Je, wewe mzazi au mlezi huoni kama una kesi ya kujibu mbele ya Mola wako Muumba?

Hawa watendaji katika Serikali, mashirika ya umma na binafsi wangekuwa wamesoma dini wakamuogopa Mola wao aliyewaumba ambaye atawauliza juu ya kila kitu, hivi wangefanya huu uharibifu unaolalamikiwa?

Tatizo hapa dini haipo kwa kuwa haikusomewa, hivyo suluhu ni kusoma na kusomesha elimu zote kwani Uislamu haubagui elimu na unalazimisha kusoma kila elimu.

Anayedhania kwamba kumlipia mtoto ada ya shule hapati thawabu, huyo hajajua vyema juu ya mafunzo ya dini ya Kiislamu katika kushughulikia dunia kwamba ukimsaidia mtu kusoma shule unapata thawabu pia.

Pia, yule anayeona kwamba shule ni lazima kusoma lakini dini atajisomesha mwenyewe kupitia magazeti na mitandao ya kijamii na hiyo itamtosha kuijua dini yake, huyo haijui dini na hajui kwamba maisha ya kidunia ni mafupi mno na ujira wa kidunia ni mfupi mno.

Haiwezekani maandalizi ya kidunia yawe ni kwa elimu ya uhakika lakini akhera iwe ni ‘ujanja ujanja’ tu, kwa hakika huyo hamdanganyi mtu bali anaidanganya nafsi yake mwenyewe.

Shime tuhakikishe kila mmoja wetu anapata elimu ya dini kwa kiwango cha kumtosha kutekeleza ibada na miamala kidini, na kama jamii tuhakikishe wanajamii wanazisoma elimu mbalimbali zinazohitajika kwa maendeleo na ustawi wa jamii.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749/ 0784 299 749



Chanzo: mwananchi.co.tz