Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taarifa ya Baraza la Maaskofu kuhusu Mwalimu Nyerere kuitwa "Mtakatifu"

3f043068643a57e640f711f08378b632 Taarifa ya Baraza la Maaskofu kuhusu Mwalimu Nyerere kuitwa "Mtakatifu"

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limesema ripoti ya mchakato wa kumwezesha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere atangazwe Mwenyeheri bado haijapelekwa makao makuu ya kanisa hilo, Vatican.

Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga alisema mchakato huo bado upo Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na TEC.

Kutangazwa Mwenyeheri ni hatua ya mwisho kabla ya kanisa hilo kumtangaza mtu kuwa ni Mtakatifu. Askofu Mkuu Nyaisonga alisema Kanisa Katoliki nchini linaendelea na mchakato huo kwa kupokea shuhuda za watu.

Alisema ripoti kuhusu Nyerere kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na TEC, haijapelekwa Roma kwa kuwa kanisa lina taratibu za kufanya mambo yake.

“Kanisa halikurupuki kufanya mambo haya na ndiyo maana kokote duniani huchukua muda mrefu, wengine hata zaidi ya karne na hata baadhi ya wenyeheri huchukua hata zaidi ya karne kabla mtu hajatangazwa kuwa mwenyeheri. Kanisa Katoliki halikurupuki,” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga.

Baba wa Taifa aliaga dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza. Oktoba 14 mwaka huu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila alisema jimbo hilo limemaliza mchakato wa ngazi ya jimbo.

Askofu Msonganzila alilieleza gazeti hili watu wengi zaidi wanaomfahamu Nyerere wapo Dar es Salaam ambako aliishi kwa miaka 40.

Nyaisonga ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, alisema kwa sasa Nyerere yupo katika hatua ya Mtumishi wa Mungu baada ya kanisa kuruhusu kuanza mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri.

Alisema jimbo husika huzingatia hoja hizo na likiridhika nazo, huomba ruhusa ya mchakato wa kumuombea kuwa mwenyeheri na ombi hilo linapokubaliwa na makao Makuu ya Kanisa (Vatican), ndipo hatua ya pili hufuata.

“Hapa, alipita maana watu ndio walisema anastahili kuwa Mtumishi wa Mungu katika kanisa kutokana na maisha na mchango wake katika maisha ya watu…” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga na kuongeza;

“Baada ya mambo hayo, kanisa (jimbo) huomba makao makuu ya kanisa, Vatican, kuruhusu kuendelea na utafiti ili akithibitishwa, atangazwe awe Mwenyeheri. Vatican ikiruhusu, mchakato huo huanza na ndipo mtu huitwa sasa Mtumishi wa Mungu na hii ndiyo hatua aliyopo sasa Nyerere.”

Alisema hatua inayofuata ni kufanyika kwa utafiti na mijadala kuhusu maisha yake kupitia kuona na kusikia shuhuda za watu wengine kutokana na miuijiza iliyotendeka kupitia maombezi yake.

Chanzo: www.habarileo.co.tz