Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAG yaomba Watanzania kuwaombea Magufuli, Samia

79cf9331685cde30af907db991a5ffaa.png TAG yaomba Watanzania kuwaombea Magufuli, Samia

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMATI Kuu ya Utendaji ya Tanzania Assemblies of God (TAG) imehimiza watanzania kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli pamoja na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe hekima na maarifa katika majukumu mazito ya kikatiba yaliyoko mbele yake.

Askofu Mkuu wa TAG Tanzania, Dk Barnabas Mtokambali alisema hayo Dar es Salaam na kuongeza kuwa kanisa hilo linatoa pole nyingi kwa mke wa Magufuli, Janeth Magufuli na familia yote kwa ujumla.

Alisema kutokana na kifo cha Rais Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu, kanisa linawapa pole pia Watanzania kutokana na msiba huo mzito na kumuomba Mungu awafariji wote na kudumisha umoja.

“Kwa hakika huu ni msiba mkubwa kwa taifa kuondokewa na kiongozi mkuu wa nchi aliyeko madarakani. Tunamuomba Mungu atupe neema ya kuvuka salama,”alisema Askofu Mtokambali.

Aidha aliwaomba washirika wote wa TAG na watanzania wote kwa ujumla kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano wa nchi hasa katika kipindi hiki kigumu kwa taifa na kuheshimu mwongozo na maelekezo yaliyopo kwenye Katiba ya Tanzania,ibara ya 37 (5) kuhusiana na tukio hilo lililoipata nchi.

Alisema ni vyema kumuombea Mama Samia ili Mungu ampe hekima na maarifa katika majukumu hayo mazito ya kikatiba yaliyoko mbele yake na kuliombea bunge ili Mungu awape hekima na maarifa wabunge katika jukumu lao la kikatiba la kuthibitisha jina la Mama Samia.

Alisema ni muhimu pia kuliombea taifa dhidi ya maadui wa ndani na nje katika kipindi hicho cha mpito ili wasije kutumia mwanya huo kuihujumu nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz