Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAG: Tumwombee Rais Samia, tuliombee taifa

91e90b6ec520a62eebebcae096612a19.jpeg TAG: Tumwombee Rais Samia, tuliombee taifa

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Askofu Mkuu wa TAG Tanzania, Dk Barnabas Mtokambali, amewahimiza Watanzania kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na taifa kwa jumla, ili Mungu ampe hekima na maarifa katika majukumu mazito ya kikatiba yaliyoko mbele yake.

Samia aliyekuwa makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2015, aliapishwa juzi kwa mujibu wa katiba kuwa Rais wa Tanzania, baada ya Rais wa Awamu ya Tano, John magufuli kufariki dunia Machi 17, mwaka huu mkoani Dar es Salaam kutokana na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Askofu Mkuu Mtokambali alisema hayo Dar es Salaam na kuongeza kuwa, Kanisa hilo linatoa pole kwa mke wa Rais Magufuli, Janeth Magufuli, familia yote na Watanzania wote kwa jumla.

Alisema kutokana na kifo hicho cha Rais Magufuli, Kanisa hilo linamuomba Mungu awafariji wote.

“Kwa hakika, huu ni msiba mkubwa kwa Taifa kuondokewa na kiongozi mkuu wa nchi aliyeko madarakani. Tunamuomba Mungu atupe neema ya kuvuka salama kipindi hiki,” alisema Askofu Mtokambali.

Aliwaomba washirika wote wa TAG na Watanzania kwa jumla, kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano wa nchi hasa katika kipindi hiki kigumu kwa taifa na kuheshimu mwongozo na maelekezo yaliyopo kwenye Katiba ya Tanzania, Ibara ya 37 (5) kuhusu tukio hilo lililoipata nchi.

Askofu Mtokambali alisema ni vyema kumuombea Rais Samia ili Mungu awape hekima na maarifa katika majukumu hayo mapya na mazito zaidi ya kikatiba yaliyoko mbele yake sambamba na kuliombea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili lizidi kufanya kazi zake kwa hekima na maarifa hususan wakati wa kuthibitisha jina la makamu wa rais mteule.

Alisema ni muhimu pia kuliombea taifa dhidi ya maadui wa ndani na nje katika kipindi hiki cha mpito ili wasitumie mwanya wa msiba huu wa kitaifa kuihujumu nchi.

“Ninaomba pia tuviombee hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili vizidi kusimamia, kulinda na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa taifa,” alisema Askofu Mtokambali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz