Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Swaumu isiyo na maadili haileti uchamungu

55326 Mawaidha+pic

Fri, 3 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwezi mtukufu wa Ramadhani umeshatukaribia. Siku chache zijazo Waislamu kila kona duniani wataanza kutekeleza swaumu ambayo ni nguzo ya nne katika nguzo tano za Uislamu.

Katika mwezi huu, Waislamu wanawajibika kufunga mchana wake wote kuanzia alfajiri mpaka magharibi. Swaumu hiyo inatakiwa ilete tija ambayo ni kumfikisha mfungaji katika daraja ya uchamungu.

Uchamungu ni tafsiri ya mtu anayeacha makatazo na kutenda maamrisho ya Mwenyezi Mungu, ambaye anasema: “Enyi Waumini mmefaradhishwa kufunga kama walivyofaradhishwa waliokuwa kabla yenu ili muwe wachamungu.”

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametamka kwamba mfungaji wa mwezi wa Ramadhani atakuwa mchamungu, huo ni ukweli usio na shaka kwamba atakayefunga atakuwa mchamungu.

Labda upande wa kuujadili na kuutilia shaka ni huu upande wa sisi wafungaji ili tubebeshwe hilo jina la ‘waliofunga Ramadhani”.

Ukweli ni kwamba upande wa sisi wafungaj, tulio wengi tumeelewa kwamba kufunga Ramadhani ni kuacha kula, kunywa na uhusiano wa kimwili kati ya mume na mke kuanzia alfajiri mpaka magharibi tu.

Swaumu na maadili mema

Ni vyema tukakubali kuacha kula na kunywa, huo ni upande mmoja wa tafsiri ya swaumu, lakini upande huo tu hautoshi kumfanya mtu kuwa mchamungu mpaka ukutanishwe na upande wa pili ambao ni mfungaji kujipamba na maadili mema.

Hivyo basi mfungaji akifunga swaumu ya Ramadhani na akatarajia afikie malengo ya swaumu yake ambayo ni kumfikisha katika uchamungu, lazima ajipambe na maadili mema.

Kuthibitisha hilo, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Swaumu sio kuacha kula na kunywa tu, bali swaumu ni kuacha pia maneno ya upuuzi na matusi”.

Akakazia tena kwa kusema: “Yeyote ambaye hawezi kuacha maneno ya uzushi na kutumia uzushi (uongo) hakuwa yeye kwa Mwenyezi Mungu na haja yoyote ya kuacha chakula chake na maji yake”.

Kwa muktadha huo, swaumu isichukuliwe ni kuacha kula na kunywa na kujamiiana tu bali ichukuliwe swaumu kwa ulazima wa kujipamba na maadili yote mema kwa ujumla wake.

Ili swaumu iwe ni swaumu kweli lazima kufunga kuhusiane na kuacha yale yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Mambo matano yanamfunguza mwenye kufunga (yanamuondoshea ujira wake): Kusema uongo, kusengenya, kufitini, kuapa kwa uongo na kutazama kwa matamanio”.

Hadithi hiyo inatuonyesha maeneo ambayo wafungaji wanapoteza fadhila za swaumu zao.

Mfungaji anatakiwa asitamke maneno ya upuuzi au maneno machafu kabisa, ndio maana mfungaji anakumbushwa kwamba ikitokea kuna mtu anamletea upuuzi au anamtukana, yeye asirejeshe na akumbuke moyoni kwa kusema kimoyomoyo “mimi nimefunga”.

Ni vyema Waislamu wote tukauonyesha umma sisi tumefunga, na kwa kuwa kufunga ni siri, swaumu itatafsiriwa na maadili mema ya mfungaji kwamba hasemi uongo, hafitini, hatukani, hadhulumu mtu kwa kumsengenya au kumsingizia lolote na kadhalika.

Swaumu itakayotuwezesha kujizuia na hayo, hiyo ndio swaumu inayotakiwa ambayo inamfikisha mfungaji katika uchamungu. Mbele yetu ipo Ramadhani ambayo tutaipokea kwa kulisikia tamko la Kiongozi Mkuu wa Waislamu wa Tanzania, Mufti Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, atakaposema mwezi wa Ramadhani umeandama basi tuamke na swaumu na uzingatie swaumu inayotakiwa ni yenye sifa za kutufikisha katika uchamungu.

Nasaha kwa Waumini

Kwanza, wanaotangaza muandamo wa mwezi bila ya kutamkwa na Mufti wa nchi waache kufanya hivyo, kwani hiyo ni fujo katika dini. Hakuna viongozi wawili katika suala la mwezi, Mufti ni mmoja tu na ndiye mtangaza mwezi.

Pili, vyombo vya habari visipokee na kutangaza muandamo wa mwezi kutoka katika vyanzo visivyo na mamlaka ya kutangaza muandamo wa mwezi. Kupokea na kutangaza ni kuwachanganya Waislamu na hayo ni matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Tatu, tujipambe kwa ukarimu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tuwakumbuke wazazi weu, mayatima, wajane, wafungwa, walemavu, wagonjwa, wanafunzi na kadhalika, tuwawezeshe ili nao wafuturu vizuri. Yeyote anayepanga kufuturu futari kumi ni vyema akapunguza mbili akampa jirani yake.

Nne, tusiwatese wafanyakazi wetu hasa wadada wa nyumbani kwa kuwatumikisha kazi nyingi huku nao wamefunga kama sisi. Tuwe na huruma na tukumbuke swaumu ni ibada inayofundisha huruma.

Tano, swaumu zetu zisiwe ni kero kwa wenzetu. Tuendeleze udugu wetu, tuchangamkiane na tufurahi kwa pamoja kwani swaumu haifundishi kununa na kupoteza uchangamfu mbele ya mwanadamu mwenzako.

Sita, tuitumie Ramadhani kwa kuomba dua, tuombe kutatuliwa shida zetu, tuwaombee wazazi wetu, ndugu na jamaa zetu wawe hai au wametangulia, tuwaombee masheikh zetu na tuiombee nchi yetu amani na utulivu.

Haya shime, Ramadhani tuifunge na tujipambe na maadili mema kwani tunayemuogopa mpaka tukaacha vyakula vyetu ili kumtii, ndiye huyo huyo aliyetuamrisha tuswali kila siku, tuache zinaa, tuache dhulma na kadhalika.

Nawatakia Ramadhani njema.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.



Chanzo: mwananchi.co.tz