Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu hatoki vinywani mwa viongozi Mbeya

49632 SUGU1+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huenda kuna walioshangaa wiki iliyopita kwa kauli ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuwa matumaini ya kulikomboa jimbo la Mbeya Mjini kutoka mikononi mwa upinzani kwenda CCM yameiva.

Imani ya Chalamila aliyoionyesha alipokuwa anapokea maandamano ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa jinsi “anavyoitendea haki Ilani ya CCM”, inatokana na kuwapo alichokieleza kama “mipango mikakati thabiti ya chama hicho ya kuhakikisha jimbo hilo linaongozwa na chama tawala.”

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na ahadi ya Chalamila kuwa, “nitaondoka Mbeya baada ya kuhakikisha wananchi wote ni kijani tena nitaondoka madarakani nikiwa tayari nimefikisha miaka 60.

Kauli hii imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Chalamila kufanya mahojiano na Mwananchi akifafanua masuala mbalimbali yanayofanyika katika mkoa huo, akibainisha kuwa upinzani katika mkoa huo ni suala la kihistoria lililotokana na tafsiri mbaya ya mfumo wa vyama vingi na watu kujiona wakongwe kama ulivyo mkoa wao.

Anasema siasa zilichukua nafasi katika mkoa huo, zikazaa kizazi kivivu na kukawa na malumbano ya kivyama.

Vilevile anasema wananchi (wa Mbeya Mjini) walizibadili kura walizopimpigia mbunge kuwa kama ndio ushindi wa kitaifa, kukawa na kizazi ambacho hakisikii na hakitulii.

“Wakawa na tafsiri isiyo sahihi kuwa kwa kuwa kiongozi ameshinda yeye ndiye alfa na omega katika kutekeleza masuala yote ya kimaendeleo,” alisema huku akihusisha hali hiyo na historia ya mkoa kabla ya uhuru.

Anasema pamoja na mkoa huo kuwa na hali ya hewa nzuri inayosapoti kilimo, ulichelewa katika ujenzi wa barabara, upangaji mji na upimaji ardhi huku siasa ikiachwa kuchukua nafasi.

Anasema hali hiyo ilisababisha mji wa Mbeya kutokutulia na uongozi ukawa mgumu.

Hata hivyo, Chalamila anasema amekuja na mfumo wa kuwaunganisha watu na makundi yote bila kujali vyama vyao, kuwaheshimu wote na kuwafafanulia dhana ya maendeleo na thamani ya kodi zao.

Huku akisisitiza uadilifu ili keki ya taifa iwe ya watu wote katika mkoa huo na viongozi kuwa waadilifu, Chalamila anamtaka mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi “Sugu” asijiite Rais.

“Mbunge usijiite rais, ni kumisbehave na ni uhaini. Hata kama watu wanakuita sisi ukatae,” anasema.

Alipoulizwa ipi ingekuwa tafsiri sahihi ya vyama vingi, mkuu wa mkoa anasema ilitakiwa iwe ni “uwezekano wa kujiunga na chama chochote na kuheshimu chama kinachoshika dola na dola yenyewe.

Kwa upande mwingine, Chalamila anasema hata CCM katika mazingira hayo walipata tafsiri isiyo sahihi ya “kuchukua kila kitu na hakuna chama kingine kinachoweza kushika dola”.

“Wakati fulani CCM haikujiandaa vizuri, walisema tutaendelea kushika dola hata kama tutakuwa na viongozi wa ovyo. Hakiko tayari kuachia dola, hakikutilia mkazo tunu za taifa, misingi ya ujamaa, Azimio la Arusha na utawala bora,” alisema.

Baada ya hali hiyo, mkuu wa mkoa anasema “CCM ilisahau kurithishana madaraka na kuandaa viongozi watakaoilinda keki ya taifa. Ufisadi, rushwa na kubebana kukatawala na viongozi wengi wamepita katika ombwe hilo la uadilifu na uzalendo.

Katika ombwe hilo, Chalamila anasema kulikosekana ajenda ya taifa ambayo inapaswa kusimamiwa na watu wote bila kujali chama na matokeo yake kila chama kina ukweli wake na hakuna ukweli wa taifa.

Matokeo yake, anasema unaibuka ubishi katika vipaumbele, kulipa kodi, mambo ambayo anapambana nayo ili kuhakikisha anaunganisha watu.

Si Chalamila pekee anayezungumzia kinachoelezwa kama athari za upinzani jijini Mbeya, hata mkuu wa Wilaya ya Mbeya,

Paul Ntinika anayesema alipofika Mbeya hali ilikuwa mbaya lakini hivi sasa mambo yanaanza kubadilika na kuwa tulivu.

Ntinika ambaye pia anakerwa na sugu kuitwa rais wa Mbeya, anasema alipoteuliwa kuongoza wilaya hiyo alikuta “hali si salama na ilikuwa haiwezekani mtu kuvaa vazi la kijani (sare za CCM) ila vazi la upande wa pili (Chadema) ndilo lilikuwa linatawala.”

“Nilikaa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kujifunza ‘hali ya usalama’ wilayani, matukio ya watu kuvamia na kupigwa...nikaanza kuifanyia kazi hali hiyo. Nikapitia viongozi wa dini tukaandaa jukwaa la pamoja, nikawa napiga maombi kama wao wakaona huyu ni mwenzetu,” anasema Ntinika.

Mkuu wa wilaya anasema kupitia mikutano hiyo na kushiriki matukio yote yanayotolea ikiwamo misiba taratibu alianza kupunguza nguvu za Sugu na upinzani.

Anasema hivi sasa hali imekuwa shwari, watu wanaweza kuvaa vazi la kijani bila ukinzani, na hata Sugu hali iliendelea kuwa tulivu.

Alipoulizwa kama moja ya kazi zake ni kuisaidia CCM ikubalike, Ntinika alisema hilo liko wazi.

“Chama kinachotawala ndicho kinatuweka madarakani na watendaji wake lazima wafanya kwa misingi hiyohiyo. Mimi ni kamisaa wa CCM, niko kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa ilani yake.”

Akaongeza, “Hii ni automatic. Ukiwa mkuu wa wilaya huwezi kuwa upande tofauti lazima ukitetee chama kwa misingi yoyote,” anasema.

Akizungumzia ushirikiano baina yake na viongozi wa upinzani, Mkuu wa wilaya anasema ni mzuri na hata madiwani, wengi wakiwa Chadema, yuko nao vizuri.

“Kwenye kata zao tunakwenda nao kwa wananchi. Tunazungumza lugha moja ya maendeleo, chama kinakuwa baadaye baadaye. Tofauti utaziona tu kwa mavazi. Hata lugha hatuwaiti upinzani au Chadema, tunasema “upande wa pili”.

Kwa upande wake Sugu anasema wanaosema umaarufu wake Mbeya umeisha wanajidanganya kwa kuwa wamezuia mikutano ya wapinzani na kuruhusu ya chama kimoja peke yake.

Anahoji kama nguvu zake zimepungua mbona anazuiwa asifanya mikutano na hata kwenda kutoa misaada?

“Majuzi tu niliomba kibali kwenda kutoa vifaa vya ujenzi wa zahanati nikakataliwa. Lakini nikaona hilo ni jambo la muhimu nikatuma msaada wangu bila mimi kuwapo,” alisema.

Kuhusu madai ya kujiita Rais, Sugu anasema yeye hajawahi kujiita hivyo, bali wananchi ndio walianza kufanya hivyo mwaka 2011 baada ya kuona alivyosaidia kutuliza mchafuko ya wamachinga yaliyowashinda viongozi.

“Hii haina maana mimi ni rais wa nchi, lakini siwezi ku-control (kutawala) hisia za wakazi wa Mbeya. Kwani ukisikia mtu anaitwa Rais wa Yanga naye anakuwa rais wa nchi, au wakati ule Lundenga, rais wa Miss Tanzania utasema naye alikuwa anajiita rais wa nchi?” anahoji Sugu.



Chanzo: mwananchi.co.tz