Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheikh Ponda atoa waraka wa Maulid, agusia...

27969 Pic+ponda TanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu wa jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ametoa waraka maalumu kuelezea mambo yanayopaswa kutafakariwa na kuzingatiwa hasa wakati huu ambapo waumini wa dini ya Kiislamu nchini wanaungana na wenzio duniani kusherekea Sikukuu ya Maulidi.

Katika waraka wake wenye kurasa 12 ukiwa na kichwa cha habari “Haki ndiyo nguzo ya amani", Sheikh Ponda ameorodhesha mambo kadhaa ikiwamo yale yanayogusu moja kwa moja imani ya Kiislam na masuala mengine ya kijamii na kisiasa.

Amesema jumuiya hiyo imeona itumie siku ya leo Jumanne Novemba 21, 2018 kutoa ujumbe wenye masilahi makubwa kwa taifa na kwa maana hiyo amezungumzia umuhimu wa Serikali kuchukua hatua katika mambo ambayo bado hayajapatiwa majibu.

Miongoni mwa mambo hayo ni yanayohusu matukio ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha akitaja pia kitendo cha kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye alitekwa hivi karibuni na baadaye kukutwa akiwa ametelekezwa karibu na eneo la Gymkhana.

“Katika yale mauaji na utekaji wenye utata, Serikali ikubali ushauri wa kuunda tume huru ya uchunguzi. Tume ishirikishe mabingwa wa uchunguzi wa ndani na nje ya nchi,” anasema Sheikh Ponda kwenye waraka huo.

Ponda amebainisha sababu za kutaka kuundwe tume huru kuchunguza matukio hayo akisema amefikia hatua hiyo kutokana na kuongezeka matukio ya utekwaji wa watu wakiwamo watu mashuhuri.

Amewataja baadhi ya watu hao ni pamoja na mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wa Kibiti mkoani Pwani, Azory Gwanda, mwanachama wa Chadema, Ben Saanane na mwenyekiti wa Halmashauri wa Kibondo, Simon Kanguye.

Katika  waraka huo, Sheikh Ponda ametaka Serikali irejeshe mchakato wa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu 2020 huku akitoa mapendekezo ya namna kutimiza ajenda hiyo.

Amesema katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mambo mengi yakijitokeza ambayo yanawafanya Watanzania kuwa njia panda hivyo jambo muhimu ili kuondoa na hali hiyo ni kurejeshwa kwa mchakato wa kupatikana Katiba Mpya.

Amesema Serikali inapaswa kuurejesha mchakato huo kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2020 na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutaliwezesha Taifa kujenga msingi mpya wa utaratibu wa kisheria na kikatiba.

“Kwa muktadha huu ni muhimu tukubaliane kitaifa kusukuma kuitishwa kwa mkutano mkuu wa Katiba. Mkutano huu uweke msingi wa kitaifa juu ya namna bora ya kurejesha mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania,” amesema

“Ni muhimu hilo kwa sababu kufanya mambo makubwa kama uchaguzi mkuu unaokuja 2020 chini ya hali ya kisiasa iliyopo na vilevile wananchi wakiwa wamechoshwa na hali hii  na bila katiba mpya au tume huru ya uchaguzi ni sawa na kuliweka taifa letu rehani,” ameongeza



Chanzo: mwananchi.co.tz