Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheikh Jongo awapa neno zito Waislamu, Dk Mwinyi aitaja amani

13406 SHEIKHE TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Kaimu Muf-ti, Sheikh Hamid Masoud Jongo amewataka Wais-lamu kutojiingiza katika mambo bila kuwa na taarifa za chanzo chake.

Alisema hayo jana wakati wa sala na Baraza la Idd el Hajj iliyofanyika katika viwanja vya Sikati Tamaa, Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Waumini wa Kiislamu waliadhimisha sikukuu hiyo ikiwa ni hitimisho la ibada ya Hija ambayo ni Nguzo ya Tano ya Uislamu.

“Mtu akaona jambo, aka-litamani halafu akaamua kuwataka Waislamu wafanye, lazima urejee kwenye chimbuko la hoja ndiyo utathibitisha uhalali wa kufanya jambo hilo,” alisema.

Sheikh Jongo alisema iwapo utataka kuharamisha jambo, basi uharamishe kwa mujibu wa rejea hizo.

Pia, alisisitiza umoja na mshikamano kwa Waislamu na Taifa katika kuendeleza amani iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa.

Sheikh Jongo alisema amani ni tunu ambayo ikiondoka haitarudi tena. “Leo hii tunao hapa viongozi wenye vyeo mbalimbali. Ingekuwa nchi nyingine isingewezekana kukaa na viongozi namna hii, ulinzi ungekuwa mkali sana, lakini sisi anayetawala na anayepinga wanapingana kwa amani na utulivu, hivi ndiyo tuendelee,” alisema.

Dk Mwinyi aitaja amani

Akizungumza katika sala na baraza hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi aliwataka wananchi kutafakari na kujifunza umakini wa kulinda amani kupitia nchi zilizopo katika machafuko.

Alitoa mfano wa jinsi wanawake, watoto na wazee wanavyoathirika katika nchi zenye vita, akisema amani ni tunu inayotakiwa kuhubiriwa kuanzia ngazi ya kaya hadi nyumba za ibada.

“Sehemu ya ujumbe wenu wa leo (jana) mliosoma hapa ni kudumisha amani, ujumbe huo Serikali ingependa kuona unafika kila msikiti, madrasa, kila nyumba ya Mwislamu na kwa jumla kila nyumba ya Mtanzania,” alisema Dk Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi katika baraza hilo.

“Amani ndiyo msingi wa kila kitu, maendeleo hayawezi kupatikana bila amani, mambo yote mazuri lazima amani iwepo kwanza.”

Alisema, “ni vyema kujifunza kutoka kwa wenzetu walio kwenye vita jinsi wanavyopata tabu na kuhangaika, hatuna budi kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani.”

Akiwasilisha salamu za Rais John Magufuli mbele ya baraza hilo, Dk Mwinyi alisema kiongozi huyo wa nchi anawaomba kuendelea kumuombea katika uongozi wake na kudumisha amani.

Dk Mwinyi alipongeza uamuzi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) wa kufanya marekebisho ya kiutendaji ikiwamo kuanza kujiendesha lenyewe kwa masilahi ya Waislamu wote nchini.

Aliiomba Bakwata kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawagusa Waislamu wote.

Alisema kaulimbiu ya baraza hilo inayosema “Jitambue, badilika, acha mazoea” inatakiwa kuonekana kwa vitendo.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka aliwataka Waislamu kuwa na umoja na kulitumia baraza hilo.

“Baraza lengo lake ni kuwaweka Waislamu pamoja. Kwa hiyo tujirasimishe na tujiweke pamoja kupitia miungano tuliyonayo maeneo mbalimbali. Tutekeleze madhumuni kwa pamoja yaliyoagizwa katika katiba ya baraza,” alisema Sheikh Mataka.

Ilivyokuwa Tanga

Sheikh Juma Luwuchu akihutubia katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa jijini Tanga, alihimiza waumini kujenga tabia ya kuwa na mshikamano pamoja na upendo baina yao ili kuwavutia wengine waipende dini hiyo.

Sheikh huyo wa Bakwata Mkoa wa Tanga, alisema ni vyema Waislamu wakaiga tabia ya Mtume Mohammad (S.A.W) ya upendo kwa kila mtu iliyosababisha watu wengi kumpenda na hatimaye kufuata dini yake ya Kiislamu. “Mkichukiana wenyewe kwa wenyewe mtawapa mwanya adui wa Uislamu kuwatenganisha na hatimaye kuipoteza dini hii ambayo ni ya haki,” alisema.

Aliwataka wanawake kutoa malezi mema kwa watoto ili kuondokana na kasi ya kuporomoka kwa maadili katika jamii.

“Ukiona kijana anavaa nusu suruali au msichana anavaa nusu uchi tambua kwamba nyumbani kwake hakuna maadili mema na ukichunguza sana utabaini mama anaona bila kukemea,” alisema.

Imeandikwa na Kelvin Matandiko na Asna Kaniki (Dar), Burhani Yakub (Tanga)

Chanzo: mwananchi.co.tz