Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheikh Gora adaiwa kutekwa Mwanza

31422 Sheikh+pic TanzaniaWeb

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mkuu wa chuo cha kidini ya Thanawi cha Nyakato Islamic Institute kilichopo chini ya Taasisi ya Elimu ya The Registered Trustees of Islamic ya jijini hapa, Sheikh Bashir Gora anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza na Mwananchi katika ofisi za Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza, katibu wa bodi wa taasisi hiyo, Sadik Mchola alisema tukio hilo lilitokea Desemba 6 chuoni hapo.

Taasisi hiyo inayomiliki shule ya awali, msingi na sekondarikuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ipo Nyakato wilayani Nyamagana.

Mchola alisema wakiwa chuoni hapo alikuja kijana kuulizia nafasi za kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya mdogo wake. “Kijana huyo alitukuta ofisini, Sheikh akamwambia aje Januari mwakani atapewa utaratibu, kijana aliondoka lakini baada ya muda kidogo akarudi tena kuulizia malipo, Sheikh akamwambia Januari ndiyo tutakueleza kila kitu, akaondoka.

“Baada ya saa moja na nusu kupita akarudi tena akasema baba amesema unipe namba ya simu, Sheikh akamwandikia akampa lakini mimi nikamuuliza unatokea wapi na unakaa wapi? akajibu natoka mtaa wa chini hapo Temeke, baba yangu amepanga hapo kuna jumba la ghorofa ila baba yangu anakaa Dar huku amekuja kikazi.”

Kwa mujibu wa maelezo ya Mchola, kijana huyo aliwaeleza kuwa yupo kidato cha tatu sekondari moja ambayo ipo mjini Bunda mkoani Mara. “Nikamwambia na wewe unaonaje ukaja kusoma hapa kwenye shule yetu, akasema sawa nitaongea na baba lakini baada ya saa moja na nusu akarudi tena na Sh10,000 kwa ajili ya kuchukua fomu ya kujiunga na shule, akapelekwa kwa mkuu wa shule.

“Baada ya hapo wakawa wanazungumza na Sheikh huku anamsindikiza kumbe walikuwa wameegesha gari yao nyuma ya chuo walipoikaribia, alitoka kijana mwingine kwenye gari hiyo wakambeba Sheikh na kumuingiza ndani kisha gari likaondoka kwa speed (mwendo) kali” alisimulia.

Mchola alisema baada ya tukio hilo walitoa taarifa polisi na wanasubiri majibu ambayo licha ya kufuatilia mara tatu wanaambiwa uchunguzi unaendelea.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema hana taarifa.

Familia yazungumza

Wake wawili wa Sheikh Gora wameelezea kwa masikitiko namna walivyopokea tukio la kutekwa kwa mume wao.

Akizungumza nyumbani kwake mtaa wa Uswahilini, mke mkubwa Safina Said alisema alipokea taarifa za kutekwa kwa mumewe saa 12:00 jioni siku ya tukio.

Alisema baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa uongozi wa chuo na hatua walizochukua, waliendelea kumtafuta kwa simu zake za mkononi lakini ziliita bila majibu hadi Ijumaa ya Desemba 7.

Alisema ana watoto saba; wa kike watano na kiume wawili, mmoja kati yao alikuwa katika chuo hicho anachofundisha mumewe.

Mke mdogo ambaye anaishi mtaa wa Nation, Farida Rashid alisema alipata taarifa za kupotea mumewe saa 3:00 usiku.

“Kwanza nilipata wasiwasi kutwa nzima sikuwasiliana naye na haikuwa kawaida yake, lakini baadaye simu ilizimika.” ila ilipofika saa tatu usiku nikaiwasha nikawapigia ndugu zake nikilalamika mbona leo hata hajanitafuta hata kunitumia sms, ndio nikaambiwa kwamba ametekwa akiwa chuoni,” alisema.

Huku akibubujikwa na machozi alisema; “Nilichofanya nilitawaza kwanza kisha nikaswali, niliishiwa nguvu kabisa.”

Wake hao wanasema hawajui cha kufanya maana wanamtegemea yeye kwa kila jambo hawana kazi yoyote wanayoifanya.



Chanzo: mwananchi.co.tz