Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yachoshwa migogoro taasisi za dini

67ea7c93ac740eb7637dd4ff3fd18aa9 Serikali yachoshwa migogoro taasisi za dini

Mon, 28 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema imechoshwa na migogoro katika taasisi za dini kwa kuwa inawagawa waumini, inahatarisha amani na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, alisema hayo jana jijini Tanga katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA).

"Naamini taasisi zote za dini zilizosajiliwa zinaendeshwa kwa kufuata katiba zilizosajiwa nazo na zina mafundisho mahususi na miongozo ya dini ambayo ina misingi katika Maandiko sasa tukiifuata, tutaweza kuepuka migogoro," alisema Dk Mpango.

Aliwataka viongozi na wakuu wa taasisi zikiwamo za dini, kuziendesha taasisi hizo kwa mujibu wa katiba zao na kwa kuzingatia mafundisho ya dini.

Dk Mpango aliwataka viongozi wa dini kuisaidia serikali kujenga jamii adilifu hususani vijana kwa kuwajengea misingi imara ya dini.

Alisema iwapo vijana wakiandaliwa vema, taifa litakuwa katika mikono salama, lakini ikiwa tofauti miaka ijayo nchi itakuwa mashakani.

Alihimiza viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi na viongozi walio madarakani ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

"Dua zenu zinatuimarisha na kutupa hamasa ya kuendelea kufanyakazi kwa uadilifu, hivyo sisi viongozi wa kiserikali tunawategemea sana nyinyi katika kututia nguvu kwenye utendaji wetu wa kila siku," alisema Mpango.

Kuhusu amani, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kukemea vitendo vya ukatili, uhalifu na uvunjifu wa maadili katika nchi.

"Niwaombe viongozi wa dini wakati mkiombea nchi yetu amani niwaombe kupitia umoja wenu hasa ili kamati ya amani ya kitaifa kuona namna bora ya kusambaza amani hiyo katika zile nchi za jirani ambazo zina uvunjifu wa amani,” alisema.

Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuber, alisema Bakwata imejipanga kutoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu, imetoa kipaumbele kwa viongozi wa dini na taasisi zake kutokana na namna inavyojiendesha kwa misingi ya haki na usawa.

"Niwasisiteze viongozi wa serikali msiwe na shaka na sisi viongozi wa dini na hata pale mnapotaka ushauri, msisite kutufuata bila ya hofu na hatuwezi kukurupuka kwani tumejaliwa hekima kubwa sana," alisema Shehe Zuber.

Kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Shehe Farid Ahmed, aliiomba serikali kuona namna bora ya kumaliza kesi zilizoko katika mahakama.

Aliishukuru Serikali kwa namna ilivyoweza kujipambanua katika kujiendesha kwa misingi ya haki na usawa.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma, alisema wamebaini migogoro mingi katika taasisi huchangiwa na kuendeshwa kwa mazoaea na kukosekana uwazi.

Alisema kuwa baraza hilo limetatua migogoro mingi na hivyo, kusaidia kuunganisha taasisi hizo katika umoja huo hali ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza changamoto zilizokuwepo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz