Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaaanza kusajili madrasa  

926047d75a467ddf946325c71c98000d Serikali yaaanza kusajili madrasa  

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza mchakato wa kusajili madrasa kwa ajili ya kudhibiti na kuweka utaratibu mzuri wa kutoa elimu ya kuendesha taasisi hizo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Kuteuliwa, Saada Mkuya aliyetaka kujua lini serikali itaanza kazi ya usajili wa madrasa.

Alisema serikali imeanzisha utaratibu huo kwa ajili ya kuzitambua madrasa na kuweka utaratibu mzuri wa kuendesha shughuli zao za kutoa elimu kwa wanafunzi.

Alisema tayari madrasa 1,011 zimesajiliwa na kutambuliwa katika mikoa ya Mjini Magharibi na Kaskazini Unguja.

Alisema usajili wa madrasa unakwenda sambamba na usajili wa misikiti katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo tayari misikiti 817 imetambuliwa.

''Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tumeanza mchakato wa kusajili vyuo vinavyotoa elimu ya Kuran yaani madrasa ambapo kazi hiyo imeanza kwa upande wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na Kaskazini Unguja. Tunaendelea na kazi hiyo,”alisema.

Awali waziri huyo alisema wizara ipo katika hatua za mwisho kutayarisha mitaala ya masomo, ambayo itatumika kwa walimu wote wa madrasa Unguja na Pemba.

Alisema mchakato huo ni muhimu na utakawenda sambamba na usajili wa walimu hao, kwa kufanya usaili ili kuwapata walimu wenye sifa watakaotoa huduma za elimu kwa wanafunzi na kuepukana na matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

''Ofisi ya Mufti ipo katika hatua za mwisho za kufanya usajili wa walimu wa madrasa ambapo suala hilo ni muhimu baada ya kubainika baadhi ya walimu wanafanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia,''alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz