Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali, viongozi wa dini wafungue ukurasa mpya

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki iliyopita Rais John Magufuli alikagua ujenzi wa msikiti mkubwa huko Kinondoni alizungumzia mambo makubwa mawili.

Mosi, aliwataka viongozi wa dini kutowatumia wanasiasa kueleza “mambo” yao na akaahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na dini zote.

Ni imani yangu kuwa alitoa maneno haya kwa moyo wa dhati na si ya kisiasa, na ndiyo maana yamerudiwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Baraza la Iddi.

Ni kweli kuna umuhimu wa Serikali kushirikiana na viongozi wa dini. Nasema hivyo kwa sababu Agosti 2016, viongozi wa dini kwa umoja wao waliomba kukutana na Serikali kuzungumzia mustakabali wa amani ya nchi yetu kulipokuwa na vuguvugu la maandamano ya Ukuta.

Sote tunafahamu na hili wala si jambo la siri, kwamba mpango wa maandamano yale ulifanya nchi ikataharuki hadi Jeshi la Polisi likaingiza vijana wake barabarani na silaha wakifanya mazoezi ya utayari.

Kauli ya viongozi hao wa dini ya kutaka kukutana na Serikali ndio iliyowasukuma Chadema waliopanga maandamano hayo kutangaza kuyasitisha wakisubiri hatima ya mkutano huo wa viongozi wa dini.

Leo hii tunaelekea mwaka wa pili viongozi hao wa pande hizo mbili hawajakutana, lakini kauli hii ya Rais ya kufungua ushirikiano na viongozi wa dini inaweza kuwa ufunguo wa ukurasa mpya.

Ni vizuri viongozi hao na wengine upande wa Serikali waone umuhimu wa kauli hiyo Rais kama baba wa familia, wafungue ukurasa mpya wa ushirikiano.

Katika mikutano hiyo ya pamoja, naamini hata ujumbe wa rais wa sasa, kwamba “viongozi wa dini msiwe na wasemaji ambao si viongozi wa dini” ungepata mahali sahihi pa kuujadili na kuwekana sawa.

Rais alisema: “Mnapokuwa viongozi wa dini halafu mkawatumia wasemaji ambao si viongozi wa dini au ni wanasiasa, mtakuwa mnachanganya dini na siasa, kitu ambacho ni kibaya sana,” alisisitiza Rais.

“Kama ni masheikh wazungumze masheikh. Kama ni Mufti anazungumza Mufti, kama ni askofu azungumze askofu na kama padre azungumze padre. Msitafute wasemaji kwa niaba yenu”

Rais alisema pale panapokuwa na wasemaji wengi katika masuala ya dini, hata yale wanayoyasema yanakosa maana, kwa kuwa haitaeleweka kama yamesemwa na viongozi wa dini au waliotumwa.

Mimi naamini, kama Rais angekutana na viongozi wa dini kwa umoja wao kuanzia Septemba 2016, naamini wangekuwa wameweka utaratibu mzuri wa namna ya kushauriana katika masuala ya kitaifa, likiwamo hili la sasa.

Ni kwa msingi huo, naamini hata waraka wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki na ule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usingebeba maudhui yale tuliyoyaona.

Lakini ni kwa sababu milango haikuwa imefunguliwa ndio maana walitumia njia ile kufikisha ujumbe wao na kueleweka kwa namna tofauti.

Tumeona wakati mjadala wa nyaraka hizo ukiendelea, wiki iliyopita Jumuiya za Taasisi za Kiislamu Tanzania, nao walitoa waraka wa Eid El Fitr 1439H/2018 uliobeba maudhui na ujumbe unaofanana nazo.

Kama ilivyo kwa maaskofu, waraka huu wa Jumuiya za Kiislamu imezungumzia kuminywa kwa uhuru wa Bunge na mahakama, uhuru wa kujieleza na hata matukio ya watu kuteswa, kuuawa na wengine kupotea.

Ni vizuri Serikali ikaelewa kuwa waumini wa dini zote wanawaamini zaidi viongozi wao, hivyo ijitahidi kushughulikia madai ya viongozi wao.

Franklin Roosevelt, aliyewahi kuwa Rais wa 32 wa Marekani (1933-1945), aliwahi kusema; “In politics, nothing happens by accident. If it happens, you can bet it was planned that way”.

Kwa tafsiri yangu, ni kwamba katika siasa hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya na kama kitatokea unaweza kubahatisha kwa kusema kilipangwa kitokee hivyo.

Serikali ielewe kuwa haya yanayotokea leo hii kwa viongozi kutoa matamko hasi dhidi ya utawala wake hayatokei kwa bahati mbaya, ifungue ukurasa mpya na viongozi wa dini.

Chanzo: mwananchi.co.tz