Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia atoa wito taasisi za dini kumega sadaka ili zichangie elimu

26709 Pic+samia.png TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za dini nchini zimege sadaka zinazotolewa na waumini ili zichangie kujenga taasisi za elimu.

Ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 12, 2018 wakati  akiweka  jiwe la msingi Katika shule ya sekondari New Dawn iliyopo Kijiji Cha Ishinde, kata ya Njoro wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema lengo la kuchangia sadaka hizo ni kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu pamoja na yatima.

"Kituo hiki ni mali ya Tanzania, hatuna budi kuchangia, tunaomba hata sadaka zinazotoka kanisani tuzimege kidogo zije hapa tusaidie kujenga kwa pamoja," amesema Samia.

Makamu huyo wa Rais ameahidi kuchangia shule hiyo ambayo itaanza rasmi mwakani na kuahidi fedha hizo atazituma mapema.

"Kituo hiki kitahudumia Taifa zima na si Same tu, elimu ni sadaka ukimpa kijana elimu itaweza kumsaidia yeye na familia pamoja na kusaidia vijana wa baadaye ambao wataweza kulisaidia Taifa letu hapo baadaye," amesema.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema eneo la shule hiyo ambayo ipo eneo la wafugaji litasaidia kunufaisha jamii hiyo ya Kimasai na kusema kila jamii inayozunguka eneo hilo ichangie ili watoto wapate elimu bora.

Naye mkurugenzi wa kituo hicho, Askofu Steven Mshomi amesema ujenzi wa jengo la shule hiyo umegharimu zaidi ya Sh700 milioni na imelenga kusaidia watoto wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu.

"Mwaka ujao tutaanza kidato cha kwanza kwani tumeshajenga madarasa manne pamoja na bweni ambalo litachukua wanafunzi 36," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz