Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu Mchungaji Kimaro kusimamishwa siku 60 yaanikwa

Kimaro  WhatsApp Mchungaji wa KKKT Usharika wa Kijitonyama, Dk. Eliona Kimaro.

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Dk. Eliona Kimaro, amesamehewa adhabu yake ya likizo ya siku 60 akiwa ameitumikia kwa siku 34 hadi jana.

Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, alitangaza msamaha huo jana.

Mch. Kimaro alikutana na msamaha huo aliposhiriki ibada ya shukrani katika Usharika wa Kinyerezi, Tabata jijini Dar es Salaam iliyoongozwa na Askofu Malasusa.

Kusimamishwa kwa Mch. Kimaro kulianza kufahamika usiku wa Januari 16 mwaka huu kupitia video iliyokuwa inasambaa ikimwonyesha akiwaaga waumini wa ibada ya masifu ya jioni, kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa kwenye ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.

Katika video hiyo, Mch. Kimaro alitangaza kumaliza likizo yake Machi 17 mwaka huu na baada ya likizo, atatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Dayosisi na sio kwenye usharika huo tena, huku akiacha sintofahamu kwa waumini bila kufahamu sababu.

Katika msamaha uliotangazwa jana wakati wa ibada hiyo, Mch. Kimaro alipewa nafasi ya kusalimia waumini hao akiwa kama mchungaji mshiriki wa ibada na ndipo alitumia fursa hiyo kuomba radhi na kueleza sababu za adhabu aliyopewa.

"Nitumie fursa hii kwa moyo wa unyenyekevu na ninasikia kunyenyekea sana ndani ya moyo wangu, kuwaomba sana radhi na msamaha kwa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa kwa mambo mengi yaliyoendelea na yaliyosikika kwenye mitandao ya kijamii na mengine hayakuwa na sura nzuri," alisema.

Mchungaji huyo alisema kuwa Novemba 13, mwaka jana, akiwa kwenye ibada ya mavuno katika Usharika wa Kijitonyama, aliongoza ibada na kuhubiri, kuwaombea wanafunzi wa kidato cha nne na vijana wasio na ajira.

"Mwishoni nilisukumwa kuwaombea wale vijana wasio na ajira na nilisisitiza suala la nidhamu, ‘Seif Discipline’ (nidhamu binafsi) na ‘life Discipline’ (nidhamu ya maisha) na katika kusisitiza, nilitoa mfano wa vijana wa usharika wangu wa Kijitonyama na wale wa dhehebu lingine, labda nitamke wazi wale wa Kiislamu.

"Baada ya hapo yale maneno yalinukuliwa kwa kukatwa huko duniani na watu nisiyowajua na kutengenezwa 'clip’ (video fupi) ambayo ilikuwa inaonyesha ulinganifu kati ya vijana wa Kiislamu na Wakristo katika suala la uaminifu hasa kwa vijana.

"Jambo hilo limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya jamii na sintofahamu, wapo waliopekea ‘positive’ (chanya) na waliopokea ‘negative’ (hasi)," alisema.

Mchungaji huyo alisema amepokea uamuzi wa Askofu Malasusa kama mchungaji mwenye kiapo na nadhiri ya daima za uchungaji, kutii maelekezo ya askofu.

"Katika nidhamu ya kanisa na agizo la kanisa, lazima viongozi wa kanisa walichukue na moja ya mambo ya misingi waliyochukua ni kupata mapumziko ya kutafakari na moja kwa moja nilipokea kwa unyenyekevu na kwenda kwenye nyumba za malezi ya kichungaji na ndiko nilipotokea asubuhi ya leo (jana), nikiendelea kusali, kutafakari na kufunga," alisisitiza Mch. Kimaro.

Aliomba radhi kwa Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Frederick Shoo kwa usumbufu aliopata wakati akiwa likizo ya siku 60.

"Ninaomba radhi kwa wakristo wote duniani, waliokwazika kwa matamshi yangu, ninaombeni sana radhi kwa hili," alisema Mch. Kimaro.

MALASUSA AMSAMEHE

Baada ya Mch. Kimaro kumaliza kuzungumza, Askofu Malasusa alisema kuwa kwa niaba ya washarika, Mch. Kimaro amesamehewa na aendelee kutafakari na kukaa karibu na Mungu ili shetani asimwondoe kwenye mstari.

"Ninaomba nikushike mkono, pole sana, sana, sana, sana, sana mama, ninajua pia umeumia sana (mke wa Mch. Kimaro), endeleeni kutafakari na kukaa chini ya miguu ya Mungu.

"Tunaiona huduma yenu na Mungu awatie nguvu, nitaendelea kuwaombea kwa sababu ni jukumu langu, nanyi bado ni watoto. Mungu awabariki sana, Mungu awatie nguvu," alisema Askofu Malasusa huku akiwashika mikono.

Wakati hayo yakiendelea, kanisa lililipuka kwa shangwe na vilio vya furaha kwa kile walichodai ni unyenyekevu alioonyesha Mch. Kimaro na ukomavu wa Askofu Malasusa kumsamehe.

BANGO MOROCCO

Saa chache kabla ya msamaha huo, baadhi ya waumini walioonyesha kuumizwa na adhabu ya Mch. Kimaro, walichanga fedha kwenye kundi songezi la WhatsApp lenye jina la ‘Bring Back Our Kimaro (Mrudishe Kimaro Wetu), walibandika picha yake eneo la Morocco, Kinondoni.

Bango lenye picha yake lenye maandishi yanayosomeka ‘But The Greatest Of This Love’ 1 Cor 13: 13 na kichwa cha habari kikubwa kinachosema ‘Let There Be Light’ ikiwa na maana 'Na iwe nuru', na ujumbe unaosema, ‘washarika na waumini wa Kijitonyama tunakupenda’.

Bango hilo lilibandika juzi jioni na watu mbalimbali walikuwa wakipita kulipiga picha na kurusha kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live