Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIKUKUU YA EID: Wafanyabiashara, wananchi wapongezana bei za bidhaa

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyabiashara katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam wamesema mwaka huu wamelazimika kupunguza bei za bidhaa katika msimu huu wa Sikukuu ya Eid El-fitir ili kuendana na hali ya uchumi iliyopo.

Wameyasema hayo leo Jumanne Juni 4, 2019 katika soko kuu la Kariakoo, Ilala na Tandika ikiwa leo ni maandalizi ya mwisho kuelekea sikukuu hiyo itakayofanyika kesho Jumatano ikitegemewa na mwenzi mwandamo.

Mfanyabiashara wa nguo Kariakoo, Stephen Mtawa amesema wameamua kufanya hivyo ili kuondoa malalamiko kwa wateja wao.

“Mteja mfalme, japo kuwa bei zetu ni zilezile za msimu uliopita lakini tumejitahidi kupunguza angalau na sisi tupate chochote maana tukisema tukomae na bei zetu nguo zitabaki nyingi stoo,” amesema.

Ameongeza, “mfano mwaka jana nguo nilizokuwa nikiiuza Sh30,000 mwaka huu nauza Sh25,000 hadi Sh20,000 hiyo ni kwa nguo za watoto, za watu wazima nauza gauni moja Sh40,000 ambapo imepungua kutoka Sh55,000 mwaka jana.”

Mfanyabiashara wa vyakula Ilala, Suleiman Khamisi amesema hali ya biashara kwa upande wa vyakula ipo kawaida huku akijivunia kupata wateja wengi siku ya leo.

Pia Soma

“Nauza mchele, viungo mbalimbali na unga japo soko la unga limetetereka kidogo leo lakini mchele na viungo ipo vizuri,” amesema.

Amesema bei ya mchele ipo kawaida ambayo kila mwananchi ana uwezo wa kununua ambapo bei zinaanzia Sh1500, Sh1700, Sh1800, Sh2000 na kuendelea kulingana na aina ya mchele.

Kwa upande wa vitoweo nyama kilo moja ni Sh5500 kwa kilo Tandika, kuku kuanzia Sh14,000 na kuendelea ambapo mfanyabiashara wa kuku Ilala, James Mwakaleli amesema bei za kuku zinatofautiana kulingana na ukubwa wa kuku.

Mkazi wa Kigamboni, Hafsa Ismail aliyekuwa sokoni Kariakoo kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu amesema anawashukuru wafanyabiashara mwaka huu kwa kujali na kuthamini hali ya uchumi.

“Sasa hivi hata ukiwa na Sh20,000 mtoto anavaa nguo ya sikukuu tofauti na miaka iliyopita ambapo bila Sh50,000 hupati nguo,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz