ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa'ichi amemuelezea Rais John Magufuli kuwa alikuwa mtu mwenye haki na amehimiza umma kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema hayo wakati wa ibada ya misa ya kumuaga Dk Magufuli aliyoongoza iliyohudhuriwa na Askofu mstaafu wa Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, mapadri zaidi ya 15 na mashemasi.
Ruwa’ichi alisema Magufuli alimpa Mungu yaliyompasa. Alisisitiza katika kipindi hiki cha maombolezo kujipa moyo kutokana na imani ambayo Rais Magufuli aliamini na kufuata.
Alisema wakati Watanzania wakimuombea Dk Magufuli, inapaswa kuombea taifa ambalo alilipenda na kulihudumia kwa nguvu zake zote liendelee na umoja, amani na utawala wa haki kwa ustawi na maendeleo ya raia wake.
“Tunapomuombea Rais Magufuli tunatambua kuwa anaye mrithi aliyeapishwa kuwa rais wa nchi na kushika nafasi hiyo ambayo siyo kazi rahisi ni jukumu zito kuhudumia raia wote kwa usawa,” alisema.
Alisema Samia alishirikiana kwa karibu na Magufuli kutokana na kuwa makamu wake hivyo hakuna mwenye wasiwasi kutokana na kuelewa na kufahamu vipaumbele vya nchi hivyo ataendeleza yote aliyoanzisha Rais aliyetangulia.
“Napenda kutoa pole kwa Rais, Mama Janet Magufuli na familia nzima, Baraza la Mawaziri, wabunge na Watanzania wote kwa msiba huu mkuu naomba kuwa na moyo mkuu katika kipindi hiki kigumu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.