Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waua watatu

49806 Pic+polisi

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibondo. Watu watatu wanaodhaniwa kuwa majambazi wameuawa na Polisi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni baada ya majibizano ya risasi usiku wa kuamkia jana mjini Kibondo, Kigoma.

Milio ya risasi ilianza kusikika saa 3:00 usiku hadi saa 5:00 usiku hali iliyosababisha taharuki kwa wakazi wa mji huo na kuanza kukimbia hovyo.

Baadhi ya mashuhuda, Richard Herman na Monica Francis ambao ni majirani na mahali watuhumiwa hao walikuwa wamepanga kuvamia, walisema ilisikika milio ya risasi mfululizo baadaye waliona maiti zikiwa nje.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kupanga kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara Ernest Gabriel na polisi baada ya kupata taarifa za siri waliwahi kufika eneo la tukio na kuyadhibiti.

Mganga mkuu wa wilaya, Dk Sebastian Kima alithibitisha kupokea miili ya watu watatu na majeruhi wawili akiwamo polisi mmoja.

Dk Kima alisema polisi huyo alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa (Moi), wakati majeruhi mwingine amefanyiwa upasuaji wa dharura hospitalini hapo.

Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa wilaya ya Kibondo, Louis Bura, alipongeza ushirikiano wa wananchi waliouonyesha na kueleza kuwa imepatikana bunduki moja.

Wakati huohuo, mtu mmoja aliyetambulika Kwa jina la Simell Oltialulu mkazi wa kijiji cha Lendikinya amefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa kwa silaha za jadi baada ya mapigano yanayotokana na mgogoro wa kugombania ardhi kati ya vijiji viwili vilivyopo wilayani Monduli, Arusha.

Pia, mgogoro huo ambao umedumu muda mrefu katika vijiji vitatu vya Lendikinya, Emairete na Arkalia ambako wananchi wa vijiji hivyo wanagombea mipaka kati ya msitu wa hifadhi ya Lendikinya.

Mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya Monduli, Dk Debora Karega alisema Machi 28 alipokea majeruhi sita kati yao, mmoja aliruhusiwa na wengine wawili wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru huku mmoja akifariki dunia asubuhi ya jana.

“Tulipokea majeruhi sita wakiwa na majeraha vichwani, mikononi na miguuni kutokana na kupigwa kwa sime, mishale na fimbo wawili hali zao si nzuri tumewahamishia hospitali ya mkoa,” alisema.

Naye mbunge wa Monduli, Julius Kalanga alisema hawajaridhika na utatuzi wa migogoro mbalimbali katika wilaya hiyo, hivyo kuwataka viongozi kila mmoja kwa nafasi yake kutekeleza wajibu wake kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika kwa kuzungumza na wananchi kwa karibu.

Akizungumzia tukio hilo, kaimu kamanda wa polisi mkoani Arusha, James Manyama, alithibitisha kutokea tukio hilo na kusababisha kifo cha mwananchi mmoja.

Manyama alisema watu wanne wanashikiliwa na polisi akiwamo diwani Bariki Sumuni na kwamba vurugu hizo ziliwahi kutokea mara ya kwanza kamati ya ulinzi na usalama ilisuluhisha, hivyo hiyo ni mara ya pili.



Chanzo: mwananchi.co.tz