Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Tanzania yazungumzia sikukuu ya Eid kwa watoto, wazazi

70987 Pic+idd

Tue, 13 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala nchini Tanzania, Alhaj Zuberi Chembela amewataka wazazi kuwa makini kwa kuwalinda watoto wao wakati wakisherehekea sikukuu ya Eid-El-Adh’aa.

Amesema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wapo salama na hawafanyi matendo yasiyo mpendeza Mungu.

Akitoa salamu wakati wa Swala ya Eid-El-Adh’aa na Baraza la Eid kitaifa iliyofanyika kwenye viwanja vya msikiti wa Kibadeni, Chanika jijini Dar es Salaam, Kamanda Chembela amesema pamoja na ulinzi huo kwa watoto, wazazi na viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kutenda matendo mema.

“Isifike mahali unamkataza mtoto kufanya jambo baya wakati wewe kiongozi na mzazi unaongoza kwa kutenda jambo baya,” amesema Kamanda Chembela

“Niwatake na niwaombe Waislamu wote msherehekee sikukuu hii kwa amani, ulinzi umeimarika na kila mahali kila kitakachotokea ambacho kitaonyesha dalili za uvunjifu wa amani kitashughulikiwa.”

Awali, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia alimpongeza Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber kwa namna alivyoweza kuwaunganisha Waislam kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza suala la uchumi.

Pia Soma

“Sisi Waislamu tumuunge mkono kiongozi wetu kwa kumtii,” amesema Mtulia.

Naye Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam akitafsiri vifungu vya Quran vilivyokuwa vimesomwa kwenye swala hiyo alisema ili uwe kiongozi lazima upite kwenye majaribu na mitihani ili jamii imuamini na kuona kuwa anastahili nafasi hiyo.

Amesema Waislam wanapaswa kuwa wamoja, kushikamana na kupendana.

Chanzo: mwananchi.co.tz