Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pasaka ni ukombozi tazama kazi ya msalaba ili upokee uponyaji na uishi

53400 Pic+mahubiri

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shaloom Shaloom wana wa Mungu, heri ya sikukuu ya Pasaka.

Jina langu naitwa Nabii Richard Godwin kutoka kanisa la Jehovah Mercy International Ministry lenye makao makuu Swaswa mkoani Dodoma.

Jumapili ya leo tumepata neema ya kukutana tena kupitia gazeti la Mwananchi tukisherehekea sikukuu ya Pasaka.

Pasaka ndiyo sikukuu yenye maana kubwa zaidi kiimani kwa Mkristo yeyote kuliko sikukuu nyingine kwa sababu hapo ndipo imani halisi ya ukombozi ilipozaliwa.

Tunaweza kusema bila Pasaka hakuna Ukristo hapa namaanisha kama Yesu asingekufa na kufufuka kusingekuwa na wokovu.

Moja ya misingi ya Wakristo ni kwamba Yesu alisulubiwa msalabani, akafa, akazikwa na siku ya tatu alifufuka kutoka kwa wafu.

Baada ya kuelezea kidogo kuhusu Pasaka, mahubiri yangu leo nataka tuangalie kazi ya msalaba kwa mwanadamu.

Katika kitabu cha 1 Petro 3:18-19 neno la Mungu linasema, “kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa ambayo kwa hiyo waliwaendea roho waliokuwa kifungoni akawahubiri.

Kwa hiyo Yesu aliteswa msalabani kwa ajili ya dhambi za mwanadamu. Tunapoangalia kazi ya msalaba lazima tuangalie ni kitu gani Yesu alikuja kufanya?

Ukisoma katika kitabu cha Luka 19:10 Biblia inaandika kuwa “Kwa maana mwana wa binadamu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea.”

Wakristo wengi tumesahau kuwa kuna kitu ambacho Yesu alikuja duniani ili kukitafuta na hicho alichokuja kukitafuta kilikuwepo lakini baadaye kikapotea.

Japo kilipotea hatuna juhudi ya kukijua ni kitu gani hicho ambacho baada ya kukitafuta nini kifanyike? Haiwezekani Yesu aje kutafuta kitu ambacho hakikuwepo kwetu. Hicho kilichotafutwa na Yesu kilikuwepo lakini kikapotea.

Katika kitabu cha Mathayo 6:33, imeandikwa “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Ufalme wa Mungu ulikuwepo tangu enzi ya Adam katika bustani ya Eden, lakini kwa makosa ya Adam ufalme wa Mungu ukapotea. Maana yake utawala wa Mungu ukapotea hivyo hivyo Yesu alizaliwa duniani kuja kurejesha ufalme ule uliopotea.

Hata ukiangalia harakati zilizosababisha Yesu afe pale msalabani ni utawala kwa sababu wengi walimhukumu kwa kujiita mfalme wa Wayahudi.

Katika kukumbuka maisha ya Yesu, kufa na kufufuka kwake, ni lazima tujadili na kutafakari ni kwa kiasi gani utawala wa Mungu upo na unatenda kazi katika maisha yetu ya kila siku.

Kama ukitawaliwa na Mungu yapo mambo mengi sana utaweza kukabiliana nayo.

Sasa katika ufalme wa Mungu ndani yake kuna nini au ni kitu gani kinachotakiwa kututawala? Biblia inasema katika Warumi 14:17, “maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika roho mtakatifu.”

Kumbe katika ufalme wa Mungu tunatakiwa kutawaliwa na haki, amani na furaha. Tunapozungumzia mambo haya katika ufalme wa Mungu tunazungumzia wizara za utendaji katika ufalme wa Mungu.

Kikawaida ukitaja haki unaigusa Wizara ya Sheria, ukisema amani unaigusa Wizara ya Ulinzi, ukitaja furaha unaigusao Wizara ya Michezo na Burudani.

Katika kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo maana yake lazima tujikumbushe kuwa tunatawaliwa na ufalme wake uliobeba haki, amani na furaha.

Kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka kiwe cha kurejesha vitu hivyo. Unatakiwa kuhakikisha unakuwa na amani moyoni mwako, samehe wale wote waliokukosea.

Kufufuka kwa Yesu kukarejeshe furaha ile iliyopotea kwako.

Hata kama ndugu zako wamesababisha furaha yako ipotee Yesu amekuja kuirejesha. Hata ndugu zako wamekupotezea furaha yako, utazame msalaba kwa sababu kupitia huo Yesu ameirejesha na utakuwa mtu wa amani.

Pasaka ni ukombozi kwa mwanadamu na ukiutazama msalaba utaishi. Yesu ameuchukua udhaifu wote, amejitwisha aibu na fedheha zote na akiwa msalabani alisema “imekwishwa.”

Ina maana kila gumu lililokuwa linakusumbua limekwisha. Kila ugonjwa, dhiki na taabu zilizokuwa zinakuandama zimekwisha kupitia nguvu ya msalaba. Msomaji wa Mwananchi, huna sababu ya kuendelea kulia na dunia kwa sababu yote alimaliza alipowambwa msalabani.

Ifanye siku hii ya Pasaka kuwa ya furaha, amani huku uzima ukiwa upande wake.

Tazama kazi ya msalaba Pasaka hii ili Yesu anapofufuka afufuke pamoja nawe. Basi kumbuka kwamba, kama Bwana alivyokusamehe wewe, wewe nawe unapaswa kuwasamehe kabisa wote waliokukosea.

Mungu akubariki sana na unaweza kunipata kwenye kurasa zangu za Facebook, Instagram na Youtube kwa kutafuta Nabii Richard Godwin

Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Mwananchi



Chanzo: mwananchi.co.tz