Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pasaka bila ya shamrashamra majumbani

102250 Pic+pasaka Pasaka bila ya shamrashamra majumbani

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya miaka mingi, Watanzania leo wanasherehekea sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo kwa namna tofauti na utamaduni wao wa kuadhimisha moja ya siku kubwa mbili kwa Wakristo duniani katika mwaka.

Wataweza kula na kunywa lakini katika shughuli zinazohusisha watu wachache na zisizo na shangwe zilizozoeleka wakati wa kusherehekea kufufuka kwa Yesu Kristo kwa matukio kama ya ubatizo ambayo hufanyika Jumatatu ya Pasaka au shughuli za kifamilia au kiukoo.

Hali hiyo inatokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, ambao hadi jana jioni ulikuwa umeshaua watu watatu nchini huku maambukizi yakifikia 32. Duniani, Covid-19 imeshaua zaidi ya watu 104,000 na kuambukiza zaidi ya watu milioni 1.7.

Wakati nchi jirani na nyingine duniani zimepiga marufuku matembezi au kutoka majumbani, Tanzania imesema hatua kama hiyo ina madhara makubwa na hivyo haitatoa amri hiyo kwa sasa.

Hata hivyo, Serikali imetangaza kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima, imefunga shule na vyuo na kuzuia shughuli za michezo na nyingine zinazovuta watu wengi, huku masharti dhidi ya vyombo vya usafiri wa umma kutojaza abiria, yakisababisha usafiri kuwa mgumu na hivyo watu kutopenda kufanya matembezi.

“Tutapika chakula kizuri, kunywa na kuvaa nguo nzuri, lakini kuepuka corona tutakaa maeneo yasiyo na misongamano,” alisema Mohamed Shibe, mkazi wa Mbagala Zakhiem.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Binafsi nitaitumia hii siku kutoa elimu kwa familia yangu kwa vitendo jinsi ya kujikinga na corona.”

Mkazi mwingine wa Kariakoo, Mbwana Yusuf, ambaye ni dereva wa bodaboda anaona hakuna ujanja zaidi ya kutii maelekezo ya Serikali.

“Pasaka ni yetu sote ila kwa mwaka huu hatuna budi kutii wito wa Serikali. Nitasherehekea nyumbani na familia yangu. Kwa watakaotoka ni bora wakawa makini sana,” alisema Mbwana.

Kauli kama hiyo aliitoa Fadhili Hamis ambaye alisema: “Hii ni sikukuu yetu na nilijipanga kusherekea vizuri ila kutokana na mwongozo kutoka serikalini, nitasherehekea nyumbani nikiwa na familia yangu. Hatuna jinsi kutokana na matatizo.”

Hata hivyo, Serikali haijazuia watu kutoka bali imeshauri wapunguze matembezi yasiyo na umuhimu katika kujihadhari na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, ambao huambukiza kwa kugusana na mtu mwenye virusi, au matone ya makohozi au chafya kumdondokea mwingine, kugusa eneo lililo na virusi hivyo na baadaye kujishika machoni, puani au mdomoni.

Serikali pia imeshauri kuwepo na nafasi ya kutosha angalau mita mbili kati ya mtu mmoja na mwingine, ushauri ambao ni mgumu kutekelezeka iwapo familia itakutana sehemu moja ya makazi.

Sherehe kubwa za mwaka kama Pasaka, pia huambatana na maonyesho ya burudani, wafanyabiashara kufungua huduma au baa mpya, bendi au wasanii binafsi kufanya maonyesho na hoteli na migahawa kutangaza shughuli maalum kwa ajili ya kuvuta wateja.

Hata hivyo, kipindi cha kuelekea Pasaka kumekuwa hakuna matangazo redioni, katika televisheni, au katika kuta za nyumba au kwa magari maalum kutangaza burudani, ikiwa ni kuitikia wito wa kuzuia mikusanyiko isiyo na umuhimu.

Hakuna bendi kuzindua albamu, au “onyesho kabambe la Pasaka,” disko toto, “ofa maalum” wala “wasanii wengi katika jukwaa moja”.

Wakazi wa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wanaona kuwepo kwa Covid-19 katika kipindi cha sikukuu hii kunawatenganisha na familia kwa kuwa wamezoea kukutana na kusherekea pamoja na familia zao.

“Watoto wangu huwa wanakuja nyumbani kusherekea sikukuu ya Pasaka, lakini kutokana na ugonjwa huu hakuna hata mmoja aliyekuja kusherekea nami,” alisema Siah Kimambo mkazi wa Msaranga.

‘’Kwa kweli huu ugonjwa ni wa kihistoria. Haijawahi kutokea hali kama hii, kwa tamaduni zetu sisi wachaga kukaa pamoja na kula pamoja wakati kama huu ni faraja sana maana watu tunachinja na kufurahi pamoja, lakini sasa hivi kila mtu yuko kivyake hatuelewi tufanye nini zaidi ya kumuomba Mungu hili janga lipite.”

Mkazi mwingine aliyeathiriwa na ugonjwa wa corona ni Adam James wa Soweto.

‘’Zamani kipindi kama hiki tulikuwa tukijiandaa na kuchagua mbuzi mnono wa kuchinja kwa ajili ya kufurahia na familia, lakini tumeshindwa kwa sababu ya hili janga,” alisema James.

“Yaani tulikuwa tunakaa pamoja na tulikuwa tukizungumza mambo mengi ya familia na koo zetu.’’

Mkazi wa Majengo, Lidya Mbwambo amekosa kutumia Pasaka kwenda kijijini kujumuika na ndugu zake kufurahia sikukuu, na badala yake watakaa nyumbani wakila na kunywa bila kutoka.

Ingawa sikukuu ya Krismasi, ambayo huwa mwisho wa mwaka, hutumiwa na familia nyingi kusafiri kwenda mikoa yao kutokana na mapumziko marefu, wengi pia hutumia Pasaka kurudi kijijini kwa mapumziko mafupi na majukumu mahsusi, lakini hali ni tofauti mwaka huu.

Hali ya watu kutosafiri kwenda mikoa ya mbali kwa ajili ya mapumziko mafupi ya Pasaka imejidhihirisha katika vituo vya mabasi.

“Tulitegemea tufanye biashara msimu huu wa sikukuu kufidia hasara tuliyoipata hapo nyuma, lakini hali imekuwa hivyohivyo, hakuna abiria kabisa” alisema Nuru Mtoto, mkurugenzi wa mabasi ya Shambalai yanayofanya safari za Dar na Tanga.

“Kutangazwa kuenea kwa virusi vya corona kumesababisha abiria kupungua.”

Iddi Shabani, ambaye ni wakala wa mabasi, alisema kuna ugumu wa biashara kutokana na idadi ndogo ya abiria hasa kwa msimu huu wa sikukuu.

“Tumezoea msimu kama huu tufanye biashara hasa kwa mikoa ya kaskazini, lakini hali imekuwa tofauti labda kidogo kwa mkoa wa Tanga gari inaweza kufika nusu,” alisema.

“Tulishazoea kipindi kama hiki ndio wakati wetu wa kupata, lakini kwa sasa si wafanyakazi wala wanafunzi ni kwamba abiria hakuna kabisa.”

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema bado changamoto ya abiria ipo kutokana na watu wengi kupumzika nyumbani ingawa ni msimu wa sikukuu.

Alisema miaka mingine kipindi kama hiki unakuta kuna msongamano wa abiria, lakini kwa kipindi hiki watu wanahofia maambukizi ya virusi vya corona.

“Tumepata athari kubwa sana hasa za kiuchumi pamoja na kipindi hiki kuwa cha sikukuu bado magari hayajai na mengine yanaondoka yakiwa tupu,” alisema Mrutu.

Suala hilo pia analiona meneja wa Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT), Maira Msana ambaye alisema hali ya usafiri haijabadilika kutokana na wengi kuelewa na kuchukua tahadhari dhidi ya Covid-19.

Chanzo: mwananchi.co.tz