Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Papa ateua Askofu Jimbo Kuu la Tabora

Papa Rugambwa.jpeg Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu Mrithi wa Jimbo Kuu la Tabora.

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu Mrithi wa Jimbo Kuu la Tabora.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima ameeleza hayo alipozungumza nasi jana.

Dk Kitima alisema uteuzi huo wa Papa umefanyika baada ya Askofu wa jimbo hilo, Paul Ruzoka muda wake wa kustaafu kukaribia.

“Askofu Mkuu Ruzoka anatarajia kustaafu ndani ya mwaka huu kwa hiyo Askofu Mkuu Rugambwa anaenda pale kujiandaa kurithi, siku Askofu Ruzoka akistaafu tu huyu anarithi,” alisema Dk Kitima.

Alisema Askofu Mkuu Ruzoka anatarajia kustaafu atakapofikisha umri wa miaka 75 ndani ya mwaka huu akiwa Askofu Mkuu wa tatu wa jimbo hilo.

Maaskofu waliomtangulia Ruzoka ni Askofu Mkuu Marko Mihayo aliyeongoza kuanzia mwaka 1960 mpaka 1985, Askofu Mkuu Mario Mgulunde (1985-2006) na Askofu Mkuu Rugambwa atakuwa Askofu Mkuu wa nne.

Dk Kitima alisema Jimbo Kuu la Tabora ni jimbo la pili kuanzishwa nchini mwaka 1878 likitanguliwa na Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambalo lilikuwa la Bagamoyo mwaka 1868.

Alisema kuanzia mwaka 1878 hadi mwaka 1953, Tabora lilikuwa jimbo la kawaida na kuanzia mwaka huo lilipandishwa hadhi na kuwa Jimbo Kuu.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, baada ya uteuzi huu anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapenda kumkaribisha Askofu mkuu Protase Rugambwa miongoni mwao kwa mikono miwili!

Hili ni Jembe la uhakika! Katika kipindi cha utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amejipatia uzoefu, mang’amuzi na utajiri mkubwa ambao sasa anakuja kuufanyia kazi kwa watu wa Mungu nchini Tanzania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lina matumaini makubwa kwa Askofu mkuu Protase Rugambwa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Rugambwa kwa sasa ni “Jembe machachari” ambalo limenolewa tayari kukabiliana na changamoto mamboleo katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baada ya uteuzi huo, alisema Askofu Mkuu Rugambwa anatarajiwa kuwasili jimboni katika kipindi cha miezi miwili baada ya likizo yake kukamilika kwa kuwa kwa kawaida askofu anapoteuliwa anakuwa na haki ya likizo.

Dkt. Kitima alisema Askofu Mkuu Rugambwa aliwahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012 alipohamishiwa Vatican.

Pia, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Congregasio ya Uinjilishaji Vatican.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live