Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padri, waumini watano wauawa kwa kupigwa risasi

57210 Pic+bukina

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watu wenye silaha wamemuua padri na waumini watano wakati wakiwa kwenye ibada katika Kanisa Katoliki mjini Dablo, Kaskazini mwa Burkina Faso, ofisa wa vikosi vya usalama amesema.

"Wakati ikielekea saa 3:00 asubuhi, huku ibada ikiendelea, watu waliokuwa na silaha waliingia ndani ya kanisa la Katoliki," alisema meya wa Dablo, Ousmane Zongo alipoongea na AFP. "Walianza kufyatua risasi na waumini kujaribu kukimbia."

Watu hao wenye umri kati ya miaka 20 na 30 kwa mujibu wa taarifa za maofisa usalama, walifanikiwa kuwakamata baadhi ya waumini, aliongeza Zongo. "Waliwaua watano kati yao. Padri aliyekuwa akiongoza misa hiyo, pia aliuawa."

Baadaye watu hao walilichoma moto kanisa, maduka kadhaa na mgahawa mdogo kabla ya kwenda kituo cha afya ambacho walikichoma pamoja na gari la muuguzi mkuu.

"Kuna hali ya taharuki katika mji huu," alisema Zongo.

"Watu wamejifungia majumbani mwao. Hakuna kinachoendelea. Maduka yamefungwa. Mji umekuwa kimya," aliongeza.

Askari wa usalama waliongezwa kutoka Barsalogho, karibu kilomita 45 Kusini mwa Dablo, na walikuwa wakifanya doria eneo hilo, ofisa kutoka vikosi vya usalama aliiambia AFP. Dablo iko katika jimbo la Sanmatenga lililoko Kaskazini.

Ikilaani shambulizi hilo, Serikali ilithibitisha kuwa waliouawa ni watu sita, akiwemo padri huyo.

Baada ya "kushindwa kugombanisha jamii kwa kufanya mauaji ya machifu na viongozi wa jamii, makundi ya kigaidi sasa yanashambulia dini katika mpango wa kutugawanya", ilisema taarifa ya Serikali.

Shambulio hilo limekuja siku mbili baada ya vikosi maalum kutoka Ufaransa kuwaachia huru mateka wanne wageni Kaskazini mwa nchi baada ya kufanya shambulio usiku lililosababisha pia wanajeshi wawili kuuawa.

Operesheni hiyo iliagizwa kwa lengo la kuwaachia huru mateka wa Kifaransa, Patrick Picque na Laurent Lassimouillas ambao walitoweka wakati wakiwa likizo katika Hifadhi ya Taifa ya Pendjari nchini Benin Mei mosi.

Timu iliyofanya operesheni hiyo pia iliwakuta mateka wawili wanawake; mmoja Mmarekani na mwingine kutoka Korea Kusini.

Shambulio hilo la Jumapili limekuja wiki mbili baada ya tukio kama hilo dhidi ya Kanisa la Kiprotestanti mjini Silgadji, wakati watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki walipomuua padri na waumini watano.

Chanzo: mwananchi.co.tz