Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padri aendesha misa ya shukurani mgodini Mirerani Tanzania

89797 Misa+pic Padri aendesha misa ya shukurani mgodini Mirerani Tanzania

Tue, 24 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Wachimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara nchini Tanzania wameshiriki misa ya shukrani kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka 2019 salama.

Paroko wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu wa Kanisa katoliki Mirerani Vincent Ole Tendeu kuongoza misa hiyo ya shukrani jana Jumatatu Desemba 23, 2019 katika mgodi wa madini ya Tanzanite California camp.

Padri Ole Tendeu akizungumza kwenye misa hiyo alisema mara nyingi watu wana tafsiri potofu kwamba wachimbaji wa madini ya Tanzanite hawapo karibu na Mungu jambo ambalo siyo sahihi.

Alisema tukio la misa ya shukrani katika mgodi imedhihirisha wachimbaji madini ya Tanzanite wana imani kubwa kwa Mungu na wanamtanguliza mbele katika shughuli zao za uchimbaji madini. 

"Misa hii ya shukrani iliyofanyika kwenye mgodi wa ndugu yetu Deogratius Minja kupitia California camp imetuonyesha imani kubwa kwa Mungu walionao wachimbaji madini ya Tanzanite," alisema Padri Ole Tendeu.

Mkurugenzi wa mgodi huo wa California camp, Minja alisema wamefanya misa hiyo ya shukrani katika mgodi huo ili kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama na kufanya kazi zao bila matatizo.

Minja alisema kazi za uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na wanamshukuru Mungu kupitia misa hiyo ya shukrani kwa kuwaepusha na ajali kwenye mgodi wao.

"Shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na zinahitaji gharama kubwa lakini tunamshukuru Mungu kwa mema yote aliyotujalia na kumaliza mwaka 2019 na kukaribisha mwaka mpya wa 2020," alisema.

Katekista wa kigango cha Mtakatifu Malaika mkuu Gabriel, Martin Mbuya alisema Mungu ni mwema kwani wamefanikiwa kuwa na eneo la kufanya ibada katika machimbo hayo.

Mbuya alisema wanamshukuru ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima kwa kuwapa fursa ya kupata eneo la kufanya ibada katika machimbo ya madini ya Tanzanite.

Chanzo: mwananchi.co.tz