Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padri Mtanzania atimiza miaka 102, asimulia siri ya kuishi muda marefu

Shayo Padre Padri Mtanzania atimiza miaka 102, asimulia siri ya kuishi muda marefu

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Heshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa Padri Louis Shayo wa Jimbo Katoliki la Moshi aliye na umri wa miaka 102, akisema vyakula pekee havitabiri mtu kuishi miaka mingi.

Padri huyo ambaye mwaka huu ametimiza miaka 70 ya upadri, anatamani Serikali ingeweka jitihada mahsusi na kuja na mpango wa kuandika vitabu vya aina mbalimbali za kilimo na kuvigawa kwa vijana ili wapate taarifa sahihi za kilimo.

Anasema anaamini kile kitendo cha kutembea umbali mrefu wa hadi kilomita 20 kwenda kutoa huduma, ndicho kilichomfanya aishi miaka mingi na kusisitiza kula vizuri haimaanishi ndio kuishi maisha marefu bali hiyo ni siri ya Mungu.

Maarufu kama Padri Lui, anaingia katika rekodi ya mapadri wachache walioweza kuishi maisha marefu na kutoa huduma ya upadri kwa miaka 70, huku akisema wapo wengi waliokuwa na afya njema walishakufa hivyo maisha marefu ni suala la Mungu.

“Siri ya mtu kuishi maisha marefu anayo Mwenyezi Mungu kwa kuwa wengi waliokuwa na afya nzuri zaidi walishakufa wakati nimekuwa nikisumbuliwa na tatizo la tumbo kwa muda mrefu,” anasema padri huyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Padri Lui ambaye sasa anaishi katika nyumba ya mapadri wazee Longuo, nje kidogo ya mji wa Moshi ni mzaliwa wa kijiji cha Imii kilichopo Kilema wilaya ya Moshi na taarifa zake za kutimiza miaka 102 zilisambaa kwa kasi mitandaoni.

Siri ya kuishi miaka mingi

Padri Lui anasema siri ya yeye kuishi miaka mingi, Mungu anajua na anasema kwa miaka yake yote amekuwa akisumbuliwa na tatizo la tumbo ambalo ameishi nalo kwa miaka mingi.

Anasema kula vizuri haimaanishi ndio kuishi maisha marefu, bali siri ya mtu kuishi maisha marefu anayo Mungu kwa kuwa wengi waliokuwa na afya nzuri zaidi yake walishakufa, huku yeye akiwa anasumbuliwa na tatizo la tumbo kwa muda mrefu.

Pamoja na hilo amesema kwa miaka yake yote amekuwa ni mtu wa mazoezi, kwani alikuwa na uwezo wa kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda kutoa huduma za kiroho kabla magari hayajaingia nchini na yalikuwa maisha yake ya kila siku.

Anasema ingekuwa chakula ndio kinatabiri maisha ya mtu yaweje huenda angekufa siku nyingi kutokana na vyakula alivyokuwa anakula, hasa kutokana na matatizo ya tumbo ambayo yamemsumbua kwa muda mrefu wa maisha yake.

“Siri ya mimi kuishi miaka mingi ni suala la Mungu mwenyewe, maana siku zote za maisha yangu nimekuwa nikisumbuliwa sana na tumbo. Chakula hakisagiki vizuri tumboni kwa hiyo mpaka leo tumbo linanisumbua,” anasema Padri Louis.

“Kuishi miaka mingi ni siri ya Mungu pekee, maana hata mimi mpaka leo sielewi. Yeye (Mungu) ndio anaweza kujibu kwa nini nimeishi miaka mingi. Kwa kweli ni Mungu pekee anaweza kujibu na hakuna binadamu anayeweza kueleza hili.”

Anasema kwa sababu ya Mungu hata anapopata tatizo kama vile kikohozi, akilamba sukari tatizo linakwisha lenyewe.

“Hata chakula nilichokuwa nakula kingenifanya mimi nife mapema, maisha yangu naishi tu kama Mungu alivyonipangia maana wapo waliokuwa na afya nzuri zaidi yangu lakini wameshafariki, hivyo mimi kuishi hivi nilivyo ni fumbo la Mungu,” anasema.

Padri Lui anasema miongoni mwa vyakula anavyopenda kula ni nyama na matunda. Amekuwa akila kwa miaka yake yote na hajawahi kula maharage kwa miaka mingi kutokana na tatizo la tumbo lililomsumbua muda mrefu.

Anachokikumbuka maishani

Katika mahojiano, Padri Lui anasema jambo kubwa ambalo hatalisahau ni wakati akisimamia gari la wananchi wakati akiwa kanisa la Kishumundu wakati huo yeye akiwa mhasibu kutokana na changamoto ya miamala ya fedha.

“Kubwa lililonisababishia na sitakaa nilisahau wakati nikiwa kwenye utumishi wangu wa upadre Kishumundu, ni kwamba nilikuwa nasimamia gari la wananchi kutoka Kishumundu kufanya biashara na mimi ndio nilikuwa mhasibu.

Anasema suala hilo lilimpa taabu kwani kuna matatizo ya maisha ambayo hawezi kuyataja lakini hilo hatalisahau.

“Kama unavyojua kazi ya uhasibu ina matatizo mengi, unaweza ukaingiziwa fedha za uongo kwenye akaunti ukaambiwa wewe ndio umezichukua, unakuta mtu anaingiza fedha na kutoa siku hiyo hiyo.

“Ukienda benki unaambiwa zimeingizwa lakini zimetolewa, kwa kweli jambo hili lilinitesa na kuniumiza sana na sitakaa nilisahau, japo changamoto za maisha ziko nyingi na zingine kwa kweli siwezi kuzitaja zinabaki siri yangu.”

Azungumzia wanaume na familia

Padri Lui anasema kwa sasa baadhi ya wanaume kwenye familia nyingi wamesahau majukumu yao ya familia na kuwafanya wanawake kuwa watumwa na kufanyiwa ukatili, akisema linapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

“Kwa mfano, sasa hivi baadhi ya wanaume tumewafanya kina mama watumwa wetu, mtu anapata mshahara anamaliza kwa matumizi yake mwenyewe badala ya kushirikiana na familia (ubinafsi), hili jambo ni baya sana na linapaswa kukemewa .

“Unakuta baba kwenye familia anatumia mshahara wake anavyotaka bila kushirikiana na familia yake na kutoa matumizi kwa familia, lakini cha kushangaza anaporudi nyumbani anadai mke ampe chakula wakati hajampa matumizi yoyote.”

“Jamii inapaswa kushirikiana kwa pamoja, hasa baba na mama katika kuwalea watoto, sasa hivi unakuta mama ndio anayelea familia baba kajiweka mbali na majukumu, jambo hili sio lenye afya, kama Mungu amewajalia watoto mnapaswa kuwalea pamoja na sio kumwachia mzazi mmoja pekee,” anasema.

Mmomonyoko wa maadili

Padri huyo anasema mmomonyoko wa maadili katika jamii unachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo suala la uchumi, akisema vijana wengi kwa sasa hawajishughulishi na kazi na badala yake wamekuwa wakikaa vijiweni.

“Baadhi wamekuwa wakikaa kwenye magenge na kupanga njama za kwenda kufanya matukio, ikiwemo mauaji na wizi na tatizo kubwa ni kukosa cha kufanya. Ipo haja kwa Serikali kutafuta namna ya kuinua uchumi kwa kundi hili.

“Tungeweza kuorodhesha watu wakapewa namna ya kujiajiri kusingekuwa na nafasi ya watu kuuana. Watu wako mtaani hawana la kufanya wanakaa kwenye magenge kutengeneza namna ya kupata fedha kirahisi,” anasema Padri Louis.

Anasema ili kuondokana na tatizo hilo, ipo haja ya Serikali kupitia wizara zake zote kuandaa vitabu vyenye mwongozo wa namna ya kujishughulisha na kilimo ambacho kimekuwa ndio mkombozi wa wengi, kikiajiri zaidi ya asilimia 70.

“Kwa mfano, vikiandikwa vitabu vinavyoelezea maana ya viwanda ili mtu akipewa mtaji ajue anafanya nini lakini mpaka sasa hakuna vitabu vya kutosha vilivyoandikwa kuwasaidia vijana kujiingiza kwenye kilimo,” anasema padri huyo.

“Tunahitaji vitabu vya kubadilisha vijana wetu, sasa hivi ukiangalia hakuna vitabu vya kutosha vya kuelezea kuhusu haya mazao yetu. Binafsi nimeona tu kitabu cha Zabibu. Nilitamani vya mahindi, mtama, maharage, ngano vyote viandikwe ambapo vitaweza kuwasaidia hawa vijana wetu, nilitamani nione hilo,” anasema.

Amzungumzia Rais Samia

Padri Lui anasema kwa kipindi kifupi Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kufanya mabadiliko makubwa sana katika sekta ya afya na elimu ambapo amesema ameweza kuboresha hospitali za mikoa nchini pamoja na shule.

“Kwa kipindi kifupi tangu Rais Samia aingie madarakani amefanya mambo makubwa, ameweka kila mkoa hospitali na shule, hakika huyu ni mama anayeona mbali. Hata namna anavyohubiri kila anapoenda nampenda sana.”

Rais Samia aliingia madarakani Machi 19 mwaka jana kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais, John Magufuli kufariki dunia jijini Dar es Salaam siku mbili nyuma.

Maisha yake, elimu yake

Padri Lui alizaliwa mwaka 1920 katika kijiji cha Imii kilichopo Kilema, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Septemba 9, 1931 alijiunga na Seminari ndogo ya St. James aliyopo wilaya ya Moshi na mwaka 1942 alijiunga na seminari kubwa.

Padri Louis anasema mzee Shayo alibahatika kuwa na watoto tisa ambapo wa kiume walikuwa watano na wa kike wanne na katika hao ana mdogo wake ambaye alikuwa ni padri na alifariki mwaka 2017.

Akizungumzia elimu, anasema wakati huo kulikuwa hakuna mpango kamili wa elimu na alibahatika kufika hadi darasa la tatu ambapo baadaye alienda seminari akiwa na miaka 11 ambapo mwaka 1931 alijiunga na seminari ndogo ya St. James iliyopo wilaya ya Moshi.

Juni 25, 1950 alipata upadri Kondoa mkoani Dodoma na baada ya kuwa padri mwaka 1950, kanisa lake la kwanza lilikuwa ni kanisa la Mashati lililopo Rombo

Licha ya kupelekwa katika makanisa mbalimbali, kanisa lake la mwisho lilikuwa kanisa la Samanga lililopo Marangu na baada ya hapo alipelekwa nyumba ya mapadri ambayo yuko hapo kwa miaka 17.

Chanzo: Mwananchi