Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padre Msimbe aeleza jinsi Papa alivyokubali Askofu Mkude ang’atuke

F20a49da209d2d1c6d433fca3825a619 Padre Msimbe aeleza jinsi Papa alivyokubali Askofu Mkude ang’atuke

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis amekubali ombi la Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude kung’atuka.

Msimamizi wa Kitume katika jimbo hilo, Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe , alisema hayo kwa mapadre na waamini wakati wa ibada ya misa ya mwaka mpya wa 2021.

"Ningependa nitoe ufafanuzi kidogo kwa sababu kuna baadhi ya mapadri wa Jimbo na hata watawa lakini hata baadhi ya waamini wananiuliza uliza maswali kwamba Desemba 30, mwaka jana (2020) ilitokea taarifa juu ya kustaafu kwa Mhashamu Askofu Telesphor Mkude " alisema Padri Msimbe na kuongeza;

"Sasa mimi nikasema toka lini Vatican wanadanganya, hiyo habari imetoka Vatican ni habari ya kweli...walipokuwa wananiuliza walikuwa wanatafuta vitu vingine , walikuwa wananichokonoa , walikuwa waliniuliza tena kwa hiyo..."

Padri Msimbe , alisema alipata barua ya uteuzi wiki mbili zilizopita kabla ya mwaka mpya kutoka katika Kongagrashio ( Idara ), inayoshungulikia uinjilishaji wa watu.

Alisema, katika barua hiyo ya uteuzi ni kwamba anapaswa kuliongoza Jimbo Katoliki Morogoro akiwa Msimamizi wa Kitume kwa kuwa sasa liko wazi.

Padri Msimbe, alisema siku za nyuma yeye alikuwa Msimamizi wa Kitume akiongoza Jimbo Katoliki la Morogoro likiwa na Askofu wa Jimbo kwa lugha ya kilatini (Sede plena).

"Nilikuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro ambalo lina Askofu lakini sasa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki ambalo halina Askofu kwa maana kwa sasa ninawajibika moja kwa moja kwa Baba Mtakatifu Vatican na kwa maana hiyo kuanzia Desemba 30, 2020 Askofu Mkude kwa sasa ni Askofu Mstaafu" alisema Padri Msimbe.

Taarifa zimeeleza kuwa, tangu Februari 12, 2019, majukumu katika Jimbo Katoliki : kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu yamekuwa yakisimamiwa na Monsinyori Lazarus Vitalis Msimbe, ambaye aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro.

Padri Msimbe alipewa jukumu hilo ili kutoa fursa kwa Askofu Mkude ashughulikie afya yake ambayo kwa miaka ya hivi karibuni ilitetereka .

Kwa mujibu wa taarifa ya Vatican kuwa, Askofu mstaafu Mkude alizaliwa Novemba 30, 1945 Pinde, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Baada ya masomo na mafunzo yake ya Kikasisi, Julai 16, 1972 alipewa daraja Takatifu la upadre Jimbo Katoliki la Morogoro.

Januari 18, 1988, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua awe Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na aliwekwa wakfu Aprili 26 , 1988 na Kardinali Laurean Rugambwa, ambaye wakati huo alikuwa Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Aprili 5, 1993, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro hadi Desemba 30, 2020, Baba Mtakatifu Francisko aliporidhia ombi la kung'atuka kutoka madarakani.

Chanzo: habarileo.co.tz