Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Pasaka ya kusonga mbele

2ca382958517d0b80561cea7a179a74b Ni Pasaka ya kusonga mbele

Sun, 4 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKRISTO wanaadhimisha Pasaka ambayo hapa nchini, viongozi wa dini ya Kikristo wamesema mwaka huu, sikukuu hii imebeba ujumbe wa kuombea zaidi taifa ili umoja, amani, upendo na mshikamano udumu na watanzania wawe na tumaini jipya.

Aidha, viongozi hao wa madhehebu tofauti , wamehimiza waumini kuwaombea hekima, maarifa na busara viongozi wapya wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyeapa hivi karibuni baada ya kifo cha Dk John Magufuli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, viongozi hao walisema pamoja taifa kuwa katika kipindi cha maombolezo ya kifo cha Magufuli, Watanzania wanapaswa kukumbuka kuwa, hakuna kipindi kinachodumu kwenye maisha ya binadamu hivyo Pasaka iwape matumaini mapya ya kuvuka katika uchungu na kuingia katika tumaini jipya.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, alisema, “Sisi kama Wakristo Wakatoliki tunapenda kutumia maadhimisho ya Pasaka hii ya aina yake kwani tupo katika mazingira ya maombolezo lakini tunapaswa kuomba amani, upendo na mshikamano”.

Aliwapongeza Watanzania kwa kuheshimu Katiba kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kupokea kijiti cha urais kwa amani na utulivu mkubwa hatua aliyosema inaonesha ni matunda ya ukombozi halisi na maendeleo ya kweli kuifuata na kuiheshimu Katiba.

“Tumempata Rais kwa kuheshimu Katiba na Rais mpya kapatikana kwa heshima ya Katiba ni Rais wa kwanza mwanamke Tanzania. Ni masikitiko na furaha ndani yake, utashi wa Tanzania kupata rais kwa utaratibu huu mzuri unatupa nguvu ya kumpa Mungu nafasi, tutii sauti ya Mungu, kuheshimu Katiba na tumpe ushirikiano Rais mpya na serikali yake,” alisema Dk Kitima.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara, alisema Pasaka hii inatoa matumaini ya uzima wa milele na ni baada ya Ijuma Kuu iliyofanyika kukumbuka kifo cha Yesu Kristo hivyo baada ya uchungu lipo tumaini jipya la furaha inayoletwa na Pasaka.

“Haya mambo mawili yanatuonesha maisha hayana upande mmoja tu wa shida, bali kuna matumaini na mafanikio, si misiba na magonjwa tu, bali kuna upande wa kufufuka, kupona na kufanikiwa hata katikati ya msiba huu wa kitaifa tuone upande mwingine wa uongozi mpya na matumaini mapya.

“Pasaka inatuonesha hakuna upande mmoja tu wa shida bali baada ya shida kuna mafanikio, kuna matumaini mapya tuzidi. Hatukai kwenye Ijumaa Kuu pekee bali kuna na Pasaka inayoleta matumaini mapya dhidi ya changamoto hizo za magonjwa na misiba,” alisema Askofu Keshomshahara.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, alisema Pasaka hii ni ya kumshukuru Mungu kwa yote na kuendelea kuomboleza pamoja na Kristo kwa kuliombea taifa.

“Kama Kristo alivyofufuka, nasi tunafufuka pamoja naye katika mahangaiko na uchungu wetu. Tufufuke naye kwa kuwaombea viongozi wapya akiwamo Rais mpya Samia aweze kufanya zaidi ya mtangulizi wake katika kuwatumikia wananchi. Tuombe kuwe na hali ya utulivu na tutakwenda salama,” alisema Kilaini.

Askofu Kilaini alisisitiza Watanzania kuwa wamoja, kusameheana, kusaidiana na kushikamana huku upendo uwe ujumbe mkuu wa Pasaka. “Tuwe na mshikamano kama Kristo alivyotufundisha, Tanzania moja tuliyoirithi kwa waasisi wetu tuilinde”.

Juzi akizungumza kuhusu Ijumaa Kuu na Pasaka, Ofisa Habari wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo, alisema uwapo wa Ijumaa Kuu unaleta matumaini makubwa kwa ujio wa Pasaka hivyo vipindi vya huzuni katika maisha ya mwanadamu haviepukiki lakini lipo tumaini katika ufufuko wa Yesu Kristo kuganga huzuni hizo.

Kwa upande wake, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa, akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu juzi katika Kanisa la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alieleza upekee wa Pasaka ya mwaka huu kwa Watanzania kwamba imeikuta nchi katika kipindi cha majonzi na utulivu baada ya kifo cha Dk Magufuli na kuhimiza waumini kumtegemea Mungu katika maisha.

Alipongeza hali ya utulivu na ukomavu wa nchi katika kipindi cha maombolezo ya kifo cha Dk Magufuli na kusema kuwa Mungu yupo juu ya taifa hili.

Alisema kupitia Magufuli, anatamani kila mtu kujifunza kwamba kinachokumbukwa kwa mtu si wingi wa miaka ya kuishi duniani au wingi wa miaka ya utumishi anayofanya bali kile anachofanya katika kutumikia kusudi la Mungu katika nafasi yoyote aliyopewa.

“Uwe kiongozi wa darasa, mwanafunzi, kiongozi yeyote. Kusudi la Mungu, umefanya nini. Wataalamu wanaoangalia maisha ya Yesu wanasema kazi ya Yesu ya kuhubiri, aliifanya katika miaka mitatu lakini mpaka leo tunaendelea kuhuishwa na maisha yake,” alisema Askofu Malasusa.

Alisema uongozi wa Magufuli ulikuwa wa pekee ambao Watanzania wana cha kujifunza. Alisema alikuwa fahari ya Afrika kwani aliweza kufanya kwa muda mfupi kitu ambacho ama kisingefanyika au kingefanyika kwa muda mrefu.

Malasusa alihimiza Wakristo kufuata mfano wa Yesu kwa kuwa watu wenye msamaha, wasiolalamika na pia kupunguza maneno wanapopitia katika hali ngumu huku akitaka wazidi kuwaombea viongozi wapya wa Serikali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz