Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabii Joshua kuongoza maelfu kuombea Taifa

5a6fa6b49df9595354b45c447e7f05f3 Nabii Joshua kuongoza maelfu kuombea Taifa

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Mwantyala ametangaza Operesheni Ombeni Bila Kukoma, iliyodhamiria kutoa dozi ya tiba kwa magonjwa yote yanayowatatiza Watanzania yakiwemo ya upumuaji katika mfumo wa hewa.

Alisema jana katika makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro wakati akizungumzia juu ya operesheni hiyo, ambayo itafanyika mfululizo ili kumweleza Mungu hitaji la Watanzania sasa.

Nabii Joshua alisema operesheni hiyo inaenda sambamba na ile ya Ombea Taifa, ambayo aliiasiwa miaka kadhaa iliyopita na imeleta mafanikio makubwa katika taifa ikiwemo kuwaponya maelfu ya Watanzania.

“Tunakwenda kuongozwa na neno la Mungu kutoka 1 Wathesalonike 5:17, Biblia inaeleza kuwa, ‘Ombeni bila kukoma’. Nasi tunakwenda kuomba bila kukoma ili Mungu wetu ambaye ndiye muumba mbingu na nchi aweze kutuondolea changamoto zote za kiafya na mambo mengine yanayotukabili kwa sasa na hakika Mungu anakwenda kujibu maombi yetu,” alisema.

Alisema operesheni hiyo, itakayoanza Februari 13 hadi 14, mwaka huu itawakutanisha maelfu ya Watanzania katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

“Tunakwenda kutumia siku mbili katika makao makuu ya nchi ili tumweleze Mungu kuwa hitaji letu kuu kwa sasa ni kuliondolea taifa letu magonjwa ya upumuaji katika mfumo wa hewa, kuuponya uchumi wetu na kuendelea kuwapa maono chanya viongozi wetu chini ya Rais John Magufuli ili waendelee kutuongoza kwa hekima na maarifa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nabii Joshua alisema huu ni wakati wa kujinyenyekeza mbele za Mungu, kwa kuwa kila amtegemeaye Mungu huyashinda mambo yote.

Alisema maelfu ya Watanzania wanatarajiwa kukusanyika katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji iliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro kwa ajili ya kuliombea taifa na viongozi wake.

Ibada hiyo itakwenda sambamba na maombi kwa ajili ya viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Nabii Joshua aliwaomba viongozi wote wa serikali kuendelea kumtegemea Mungu kwa kila jambo wanalotaka kulifanya katika taifa kwa kuwa moyo huo unawashangaza maadui wengi, ambao wanainenea mabaya Tanzania.

“Katika kitabu cha Yeremia 33:3, Biblia inasema, niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. Maneno haya ni Mungu aliyazungumza kwa kinywa cha Yeremia, alipokuwa katika gereza alilokuwa amefungwa, wakati huo Mji wa Yerusalemu ulikuwa umeshazungukwa na majeshi ya Nebukadneza na ndani ya mji kuna njaa kali,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz