Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wa Frank waendelea kusota mochwari

27228 Mwili+pic TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Licha ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kutupilia mbali rufaa iliyokatwa na ndugu wa marehemu Frank Kapange (21) waliogomea kuuchukua kwa ajili ya maziko, bado mwili huo haujazikwa. Jana, Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ulisema bado unaendelea kuuhifadhi mwili huo kwa sababu ndugu hawajajitokeza kwenda kuuchukua na hospitali haijapata maelekezo yoyote yale hadi jana mchana. Juzi mchana, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya iliitupa rufaa ya kesi hiyo iliyokuwa imekatwa katika mahakama hiyo na na ndugu wa Frank dhidi ya Jeshi la Polisi ya kuiomba kutengua uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya ambayo ilitupilia mbali maombi yao waliyowasilisha mahakamani hapo. Akizungumza na Mwananchi jana mchana, Ofisa Uhusiano wa Umma Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Arcad Mosha alisema hadi jana mchana walikuwa hawajapokea maelekezo yoyote ya tofauti wala hakuna mtu aliyekwenda kutaka kuuchukua mwili wa kijana huyo ikiwa ni siku ya 163 ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo. “Mwili bado upo mochwari tunaendelea kuuhifadhi na hatujapokea barua wala maelezo yoyote ya tofauti  kutoka kwa mtu yeyote,” alisema Mosha. Frank alifariki dunia Juni 4, huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika soko la Sido jijini hapa, alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa Polisi hivyo ndugu waligoma kumchukua na kwenda kumzika huku wakiwatuhumu polisi kuhusika. Agosti 24 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa  Mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank kuchukuliwa na ndugu ili ukazikwe na ndugu zake, baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo chake baada ya kuridhika na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa Serikali. Hata hivyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo hivyo wakaamua kukataa rufaa Mahakama kuu Kanda ya Mbeya ambayo jana ilitoa uamuzi wake wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kufungua kesi hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz