Dar es Salaam.Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Mtume Boniface Mwamposa amesema watu wasione aibu kuvaa barakoa(mask) wanapokuwa kanisani hivyo wanatakiwa kuvaa ili wajilinde na ugonjwa wa corona. Mwamposa amezugumza hayo wakati wa ibada ya pasaka amesema unapovaa barakoa kanisani siyo kwamba hauna imani hivyo lazima ufuate maelekezo yaliyotolewa na Serikali jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo. Amesema ukimuona mtu amevaa barakoa kanisani siyo kwamba hamuamini Mungu bali anajikinga na corona usione haya kuvaa unapokuwa kanisani au barabarani lazima mfuate masharti kama Serikali inavyosema.
"Usimjaribu Mungu wako kwa kusema eti umeokoka huwezi kufuata maelekezo ya Serikali jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa corona hivyo utakufa lazima ujikinge huku ukimuomba Mungu atuepushe mfano tumeona leo kila muumini anakaa mita moja kutoka kiti kingine hivyo hivyo mnapokuwa nyumbani mnatakiwa mkae mbalimbali, kunawa mikono na kutogusana," amesema Dk Mwamposa.
Pia amesema siku ya ufufuko wa Yesu kristo kila mtu aliyekuwemo kwenye ibada hiyo watafunguliwa mambo mbali mbali ikiwemo wagonjwa watapona na watu watafunguliwa kiuchumi, kikazi na kielimu.