Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume aenda kortini kudai haki ya kuzika mkewe

24942 Mume+pic TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mgogoro wa kugombea mwili wa Fatuma Assey (56), aliyefariki Oktoba 25, umetua mahakamani kati ya mume na familia ya mwanamke huyo, huku mumewe akitaka apewe haki ya kumzika mkewe.

Kutokana na ndugu wa familia ya marehemu kumzuia mume kuchukua mwili wa mkewe, mwanamume huyo mkazi wa Himo wilayani Moshi, Zuberi Shango amekimbilia mahakamani akiomba apewe haki ya kumzika.

Mwili wa marehemu umetimiza wiki moja ukiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kilema.

Katika kesi aliyofungua, mume amewashtaki wanafamilia wawili ambao ni Ausen Nkya kama mujibu maombi wa kwanza na Lodriki Kileo ambaye ni mjibu maombi wa pili.

Kwa mujibu wa maombi hayo namba 24 ya 2018 yaliyowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi juzi, Shango anadai alifunga ndoa na Fatuma, Julai 20, 2005 huko Tunduma mkoani Mbeya.

Wawili hao walifunga ndoa ya Kiislamu na hati ya ndoa namba 6306 ilitolewa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Mbeya na ikisimamiwa na Sheikh Idrisa Adeny.

“Kabla ya kufunga ndoa hii, mke wangu alikuwa akijulikana kwa jina la Betty Assery Kileo, jina ambalo alipewa na wazazi wake na ndilo linaloonekana kwenye cheti chake cha kuzaliwa,” alieleza Shango.

Katika hati hiyo ya maombi iliyowasilishwa na Wakili Mussa Mziray, Shango anadai wajibu maombi wanamzuia asimzike mkewe kwa hofu kuwa iwapo akimzika kwa imani ya Dini ya Kiislamu atakuwa na haki ya kurithi mali za marehemu.

Fatuma alikuwa ni mfanyabiashara wa mazao kwenda nchi jirani na anadaiwa pamoja na mali zingine anamiliki nyumba yenye thamani ya Sh80 milioni katika mji mdogo wa Himo.

Kesi hiyo iliyowasilishwa chini ya hati ya dharura imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Bernadetha Maziku.

Jana kesi hiyo ilipoitwa mbele ya Hakimu Mziku, Wakili Godwin Sandi anayewatetea wajibu maombi aliomba muda zaidi wa kuwasilisha kiapo kinzani kwa vile ndiyo kwanza alikuwa amepewa hati ya maombi hayo.

Wakili Sandi aliiambia Mahakama kuwa waleta maombi walikuwa wamempatia hati ya madai yao dakika 30 kabla ya kuingia mahakamani, hivyo alikuwa hajapata muda wa kuwasilisha majibu ya kiapo chao.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Tumaini Materu ambaye ni miongoni mwa jopo la mawakili watatu wanaomwakilisha mume wa marehemu alitaka Wakili Sandi awasilishe majibu hayo kwa mdomo.

Wakili Sandi aliikataa hoja hiyo na kueleza kuwa kwa vile mleta maombi amewasilisha kwa maandishi, yeye pia atafanya hivyo kwa maandishi badala ya kuwasilisha kwa mdomo.

Hakimu Maziku anayesikiliza kesi hiyo alimpa Sandi muda wa kuanzia jana saa nane mchana hadi leo saa 4:00 asubuhi awe amewasilisha majibu hayo na kesi ya msingi itasikilizwa kesho saa 6:00 mchana.

Migogoro mingine iliyotikisa Moshi

Oktoba 2014, uliibuka mgogoro wa kugombea maiti ya Rosemary Marandu kati ya mama yake, Felicia Nkya na baba, Flavian Marandu.

Mbali na kuwahusisha wazazi hao kwa upande mmoja, lakini ulimhusisha mume wa marehemu, Sigfrid Mlingi na kusabababisha mwili wake kukaa mochwari kwa zaidi ya siku 54.

Septemba 1,2014, uliibuka mgogoro wa kugombea mwili wa Steven Assey kati ya mke wa ndoa, Lucy Lawrence na mwanamke aliyekuwa akiishi na Assey, Fortunata Lyimo.

Marehemu alifariki dunia Septemba 1, 2014 kwa maradhi ambayo hayakutajwa mahakamani na kuzikwa katika Kijiji cha Masaera, Kata ya Kilema Kusini, Moshi Vijijini.

Mwaka 2003, uliibuka mgogoro wa kugombea maiti kati ya Cecilia Marandu na Thomas Marandu dhidi ya Lucresia Marandu aliyekuwa akitaka haki ya kumzika mumewe Donasian Marandu.

Mke wa marehemu akiungwa mkono na watoto wa marehemu walitaka azikwe eneo la Karanga Katanini mjini Moshi, wakati ukoo wa Marandu na Cecilia wakitaka azikwe Keryo, Rombo.

Mwili wa marehemu ulikaa chumba cha maiti cha Hospitali KCMC kwa zaidi ya siku 100, ambapo mjane alikuwa akitetewa na wakili Apolo Maruma, huku ukoo ukitetewa na Anzamen Shayo ambaye sasa ni marehemu.

Katika uamuzi wake baada ya kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Moshi wakati huo, Ignas Kitusi ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania alimpa ushindi mke wa marehemu, Lucresia.

Chanzo: mwananchi.co.tz