Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muislamu anaishi kwa lengo mahsusi

38376 MUILAM+PIC.png Muislamu anaishi kwa lengo mahsusi

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uislamu unamtaka kila Muislamu aitakidi (aizingatie) imani ya Kiislamu kuwa: Hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo ijulikanayo kama shahada ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu. Ni rahisi kutamka maneno haya, lakini kuyatekeleza katika vitendo ambao ndio ukamilifu wa Uislamu, ni shida kwa watu wengi.

Katika Uislamu, kumuabudu Allah ni kila kitendo miongoni mwa vitendo vifanywavyo na binadamu katika kutekeleza Uislamu na hata kuleta maendeleo duniani.

Iwapo imani hii itajikita katika moyo wa Muislamu na ikawa ndiyo lengo la maisha yake kama alivyotaka Mwenyezi Mungu na akafanya hivyo kwa kutafuta radhi zake pekee, mwanadamu mwenye imani hii ataleta mabadiliko makubwa duniani.

Hakika lengo la matendo ya kiibada ya mwanadamu ayatekelezayo kila siku kwa mujibu wa sheria ya Mwenyezi Mungu iliyokuja katika Qur’an na Sunnah, ni kielelezo cha jinsi Muislamu anavyoyaendea maisha yake ya binafsi, familia na kijamii.

Hakika Muislamu huhisi kwamba ibada zake hazikukamilika pindi anapokuwa hatumii juhudi na maarifa yake yote kulifika lengo la kuishi kwake duniani ambalo limeelezwa katika Qur’an 51:56.

Tutalifikiaje lengo la uhai?

Kwa mtazamo huo hapo juu, Muislam huishi akiwa na utambuzi wa kweli kwamba yeye ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu aliyeumbwa kwa lengo kuu la kumuabudu Yeye pekee.

Muislam daima hujihisi kuwa yeye ni sehemu ya ujumbe (Risaalah) wa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) ambao unamtaka kila Muislamu kuutekeleza Uislamu katika nyanja zote za maisha.

Bila kuishi kwa staili hiyo, Uislamu wake haukamiliki na wala ibada zake haziwezi kuwa na athari njema kwa jamii anayoishi nayo akiwa kama balozi wa Uislamu.

Ni pale anapoishi maisha ya kutenda mema kwa wanadamu na viumbe wengine, ndipo mwanadamu anapokuwa kama alivyokusudiwa awe na Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na kwa hakika nimewakirimu wanadamu na nimembeba (kwa vipandwa) katika nchi kavu na baharini na nimewaruzuku kwa vitu vizuri vizuri na nimewafadhilisha juu ya viumbe wengi niliowaumba kwa fadhila kubwa” (Qur’an 17:70).

Kwa hiyo Muislamu anapaswa kuwa mkweli kuhusu lengo hili tukufu na aifungue akili yake na kuviachia vipaji vyake viifanye kazi ya kuutafsiri Uislamu kwa vitendo vyema katika jamii akitumia kila alichopewa na Mwenyezi Mungu.

Hiyo ndiyo sifa yake katika dunia na ndiyo maana ya uwepo wake. Maisha pasina hali hii hayana utamu wowote hata kama ataogelea katika neema na wala hatokuwa na utulivu wa nafsi na wa kijamii nje ya maisha haya ya kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa Muislamu hiyo bado kwake ni ibada kubwa anayojikaribisha nayo kwa Mola wake ili azipate radhi zake. Ndiyo maana Muislamu wa kweli atatumia kila pumzi, nguvu na juhudi zake kuhakikisha anaishi maisha ya Risaalah.

Qur’an ndiyo chimbuko la imani

Muislamu anahitaji kufanya upya imani yake kila siku na kuilinda isimomonyolewe na harakati za maisha za kutafuta riziki na kutekeleza majukumu mbali mbali ya maisha na yale ya kijamii.

Nyenzo mojawapo ya kumkumbusha Muislamu Risaalah ya Mtume wake ni kuisoma Qur’an kila siku na kufahamu maana yake.

Qur’an ndiyo chemchemu ya mwongozo kwa muumini Muislamu na ukumbusho kwa wanadamu. Ndani ya Qur’an kuna heri nyingi na mambo ya kuifikirisha akili ya mwanadamu ili ifanye kazi barabara.

Ni bahati mbaya kwamba sisi Waislamu wa zama hizi hatujajua fika thamani ya Qur’an katika maisha yetu. Waislamu waliotangulia walizidisha sana kuisoma Qur’an na wakavuna kutoka humo utulivu wa nafsi na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Sisi tusioisoma Qur’an badala ya kumtegemea Mwenyezi Mungu katika maisha yetu tunamtegea. Maana yangu ni kwamba tumekuwa watu wa kusema; “Mwenyezi Mungu hakupenda” hata pale tunapoonja madhara au matunda ya uzembe na uvivu wetu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Wale walioamini na nyoyo zao zikatulizana kwa ukumbusho wa Mwenyezi Mungu, jueni kwa ukumbusho wa Mwenyezi Mungu ndipo nyoyo hutulizana” (Qur’an 13:28).

Muislamu mcha Mungu mwenye kujitambua, anapaswa kujipamba na sura nzuri ya msomaji wa Qur’an ambaye Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) alimuelezea.

Anasema Mtukufu wa daraja: “Mfano wa muumini ambaye anaisoma Qur’an ni kama mfano wa madanzi mwitu, harufu yake ni nzuri na ladha yake tamu. Na mfano wa muumini asiyeisoma Qur’an ni kama mfano wa tende, haina harufu na ladha yake tamu.

Anaendelea: “Na mfano wa mnafiki ambaye anasoma Qur’an ni kama tunda la rihani, harufu yake nzuri lakini ladha yake chungu. Na mfano wa mnafiki asiyeisoma Qur’an ni kama tango mwitu, halina harufu na ladha yake ni chungu.” (Bukhari na Muslim).



Chanzo: mwananchi.co.tz