Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mufti Zuberi awataka waumini wa Kiislamu kushiriki sensa

Muftipicc Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwaelimisha waumini juu ya umuhimu wa sensa nchini.

Amewataka viongozi hao kuwaelimisha waumini kuwa sensa inakubalika katika dini, pia amewataka kuwaelimisha waumini hao umuhimu wa kuchanja na njia za kujikinga na Uviko-19.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Oktoba 30, 2021 Mufti Zubeir amesema sensa katika uislamu inakubalika hivyo maneno yanayosemwa kwamba ni haramu yapuuzwe.

"Natumia fursa hii kuwaagiza masheikh wote nchini na viongozi wengine watoe elimu kuhusu sensa kwamba inakubalika katika uislamu hivyo watumie mikusanyiko ya kidini na hadhara mbalimbali, misikitini, vyuoni na sehemu mbalimbali katika kuwahutubia na kuwaelimisha.

"Sensa ni jambo zuri na lenye maana, na katika uislamu hakuna mahala ambapo hawajazungumza habari za sensa, hata katika vitabu vingine tumesoma vimezungumza habari hizi. Hata Mtume alitumia sensa kujua jeshi lake lina watu wangapi, hivyo wanaosema sensa haifai ni kutokana na elimu ndogo tu," amesema.

Kuhusu Uviko 19 alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta ufumbuzi wa ugonjwa huo kwa kuleta chanjo na kuitoa bure.

"Corona ni adui mkubwa na ni adui wa ulimwengu mzima hivyo kuiachia nafsi yako iangamie ni kujitakia kifo wewe mwenyewe. Kwahiyo masheikh watumie fursa walizokuwa nazo kuwaelimisha waislamu juu ya kujikinga na Uviko 19 kwa kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, pia kuwahimiza," amesema Mufti Zubeir.

Chanzo: mwananchidigital