Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mufti: JPM alishiriki vizuri maendeleo ya Waislamu

5f5a53f54560ff1310b401812358b774.jpeg Mufti: JPM alishiriki vizuri maendeleo ya Waislamu

Sat, 27 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MUFTI Mkuu wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi amesema Rais John Magufuli aliwapenda viongozi wote wa dini na alishiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo za Waislamu.

Alisema hayo jana mjini Chato wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na taasisi za dini ya Kiislamu nchini katika Ibada ya Maziko ya Magufuli iliyofanyika katika makazi ya familia yake.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

“Katika moja ya sifa zake kubwa alizokuwa nazo na alizotuonesha katika kipindi chote cha uongozi wake, ni mapenzi makubwa kwa viongozi wa dini; aliwatanguliza na kuwapenda na alikuwa hakosi kuwaalika katika shughuli yake yoyote anaiyofanya. Iwe ikulu au nje ya ikulu, alikuwa akiwahitaji sana viongozi wa dini kwa hili tumefarijika sana katika kipindi chote cha utumishi wake,” alisema Mufti.

Alisema pamoja na hayo amefanya mambo makubwa kwa Waislamu. “Kama nisipoyagusa nitakuwa simtendei haki Dk Magufuli; ana mambo mengi ambapo leo hakuna nafasi ya kutosha kuyataja.”

Mufti Zuberi alisema miongoni mwa mambo hayo, ni kitendo cha Rais Magufuli kuwapa msikiti unaoitwa Msikiti wa Muhammad wa Sita Bakwata ambao ni mkubwa na wenye uwezo wa kuingia waumini wengi.

Alisema hata wakati wa ujenzi wa msikiti huo, Magufuli alikuwa akifuatilia hatua kwa hatua ujenzi wake na mara nyingi aliwatuma watumishi wake kwenda kuona hatua uliofikia.

“… Alinipigia simu ghafla tu na kuniambia tukutane msikitini au njoo Ikulu tutoke wote twende msikitini tukaangalie hali ya maendeleo ya msikiti… Kwa kweli ni faraja kubwa, ni jambo kubwa kabisa lenye kujaa matumaini na kuthibitisha upendo na mahaba makubwa kwa watu wa dini bila ubaguzi,” alisema.

Mufti Zuberi alisema pia alichangisha fedha za ujenzi wa Msikiti wa Dodoma Chamwino na kwa mapenzi yake makubwa akataka uitwe Msikiti wa Shehe Aboubakar Zuberi.

“Nakumbuka aliwahi kusema, ‘siku nyingine nitakapokuwa naanza safari za kwenda nje nitakuchukua Mufti katika zile nchi unazozitaka nikakusemee zile shida na hoja zako unazozitaka.’ Hayo yalikuwa ni mahaba makubwa sana,” alisemaMufti.

Alimuombea Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi mafanikio kuiongoza Tanzania kwa usalama na amani kuelekea maendeleo zaidi.

Aidha, aliwataka wananchi, kujenga mshikamano, umoja, ushirikiano na upendo kama urithi aliouacha Magufuli.

“Kwa niaba ya Bakwata na taasisi zote za Kiislamu, tunakuhakikishia kuwa tutakuwa pamoja kuhakikisha maendeleo ya nchi hii yanapatikana kupitia vyombo vya dini,” alisisitiza.

Alisema amepokea salamu za viongozi mbalimbali wa Dini ya Kiislamu akiwamo Mufti wa Uganda, Kenya, Morocco, Mafia, Saudi Arabia, Mauritania, na nchi zote za Afrika Magharibi na Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Taasisi ya Mfalme wa Morocco Muhammad VI.

Chanzo: www.habarileo.co.tz