Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere

79843 Nyerere+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Oktoba ni mwezi ambao Watanzania humkumbuka Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania, aliyezaliwa mwaka 1922 na kufariki dunia Oktoba 14, 1999 akiwa na umri wa miaka 77. Mwalimu Nyerere anatambuliwa na jamii ya Watanzania kuwa ni tumaini la umoja na amani ya Tanzania.

Watu wenye mapenzi mema wa Tanzania na dunia nzima humkumbuka Mwalimu Nyerere kama Kiongozi mashuhuri ‘Mwana wa Afrika’. Siku ya tarehe 14 ya Oktoba 2019, Watanzania tutaungana kama Taifa moja kumkumbuka Baba wa Taifa letu.

Siku hii tutamkumbuka kwa vituo vya televisheni kuonyesha hotuba alizowahi kutoa Baba wa Taifa katika uhai wake. Magazeti pia yatachapisha matoleo maalum kukumbuka siku hii muhimu ya kiongozi wetu mkuu na Mwalimu wetu.

Wale walioishi na kufanya kazi na Mwalimu Nyerere ni mashahidi wa maisha ya Mwalimu Nyerere yaliyoonyesha uadilifu wa maisha yake katika kazi za uongozi wa Taifa la Tanzania. Alikuwa kiongozi mwema na mwenye huruma aliyeishi maisha ya kawaida akijali zaidi masilahi ya Taifa. Alifanikiwa kuijenga Tanzania moja ambamo watu wake wanaishi kwa umoja bila kujali uwepo wa makabila zaidi ya 120, watu wa dini na rangi mbalimbali.

Mara nyingi watu husema dini na siasa haviwezi kuchanganywa, lakini maisha ya uongozi ya Mwalimu Nyerere yanadhihirisha kuwa aliweza kuwa mcha Mungu na pia kiongozi mwadilifu wa Serikali yake.

Dini yake haikumzuia kutekeleza wajibu wake wa kisiasa ipasavyo. Alipowasha Mwenge juu ya Mlima Kilimanjaro alisema, “…Sisi tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka; ulete tumaini pasipo na matumaini; upendo pasipo na upendo; na haki palipo na uonevu…”

Pia Soma

Advertisement
Maono ya Mwalimu Nyerere yanayoelezwa katika maneno hayo yalikuwa ya kisiasa lakini pia ya kidini na yalidhihirika pale ambapo, Tanzania ilijengeka kuwa Taifa lenye amani, na nchi ya kukimbiliwa na watu wa nchi za jirani walipokosa amani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Tanzania ya Mwalimu ilileta matumaini pale ambapo hapakuwa na matumaini nje ya mipaka yake.

Mwalimu Nyerere alijitolea kuongoza katika kupigania Uhuru wa nchi za Msumbiji, Angola, Namibia, Zimbabwe, na Afrika Kusini, akaleta matumaini na utu nje ya mipaka ya Tanzania kwa wale walionewa na kukandamizwa na ukoloni na ubaguzi wa rangi. Leo hii Tanzania ni kisiwa cha amani kwa sababu ya Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere alikuwa Mkristo Mkatoliki, mpole na mtu wa kawaida ambapo cheo chake cha urais hakikumpa kiburi cha kubagua, kunyanyasa na kutesa watu wa Taifa lake na mataifa mengine.

Mwalimu Nyerere alipinga vita hadharani uonevu kwa maskini na wasio na mali. Pamoja na kuwa alikuwa Rais mwenye kazi nyingi aliishi kama Mkatoliki wa kawaida akihudhuria Ibada ya Misa Takatifu na kupokea Komunio Takatifu. Pia, alifunga wakati wa Kwaresima akisali na kuomba kwa ajili ya Taifa na watu wake.

Mpango wa Kanisa Katoliki wa kumuweka kwenye mchakato wa kuwa Mtakatifu ni ushahidi wa maisha ya Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa Kiongozi mwema na mwadilifu. Tabia yake ya uadilifu, uaminifu, unyenyekevu na kupenda watu umemstahilisha kuingizwa kwenye mchakato huu wa kuwekwa kwenye orodha ya Watakatifu wa Mungu.

Hatua ya kwanza katika mchakato huu wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu ni kufanya uchunguzi wa maisha yake ya kawaida.

Mashahidi mbalimbali waliitwa na kuombwa kutoa ushuhuda chini ya usimamizi wa Jimbo Katoliki la Musoma. Shuhuda hizo lazima zioneshe tabia ya kiroho ya ushujaa, imani, matumaini, na wema, lakini pia tabia ya uadilifu, haki na tabia zingine za maisha ya imani. Mwalimu alifaulu mtihani huo na akastahili kuwa Mtumishi wa Mungu.

Tabia hizo njema za Mwalimu zitapitishwa tena katika uchunguzi wa Kamati ya Kipapa ya Theolojia na ni lazima matendo yake hayo yaambatane na muujiza unauhusishwa naye baada ya kifo chake. Na kama atapita mtihani huo Mwalimu atatangazwa kuwa Mwenye Heri.

Baada ya Mwalimu kupewa cheo cha kuwa Mwenye Heri, itahitajika utokee muujiza wa uponyaji utakaothibitishwa kuwa ulitokea baada ya maombi yaliyoelekezwa kwa Mungu kupitia kwa Mwenye Heri Julius Kambarage Nyerere. Baada ya hapo atatangazwa kuwa Mtakatifu.

Mchakato wa kuwa Mtakatifu huwa ni mrefu na mgumu sana, na unaweza kuchukua karne nyingi kukamilika lakini tendo la kuwepo kwa mchakato huu ni heshima kubwa ya kumuenzi Baba wa Taifa na heshima kubwa pia kwa nchi yetu ya Tanzania. Watanzania kwa ujumla wetu bila kujali tofauti zetu za kiimani ni lazima tufurahi na kwenda pamoja kwa heshima ya Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwandishi ni mbunge na kamishna wa madini mstaafu.

Chanzo: mwananchi.co.tz