Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania aliyeibuka mshindi wa kwanza kimataifa kuhifadhi Quraani asimulia safari ilivyokuwa

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mwingine mafanikio ya mtu hayaji kwa nguvu zake pekee, bali juhudi za aliye nyuma yake huweza kuzaa matunda yanayoweza kuonekana.

Japokuwa ni ngumu kuamini kuwa mtu mwingine anao uwezo wa kukusukuma kwa kasi kubwa hadi kufikia mahala pazuri lakini suala hilo lipo na linawezekana.

Moja ya sababu za hilo kutokea ni baada ya kuona kitu ikiwamo kipawa kilicho ndani yako ambacho wewe haujakiona na ni ngumu kukigundua kwa wakati husika.

Hilo limedhihiri katika fainali za tuzo za 27 za kimataifa za kuhifadhi Quraan tukufu ambapo Zakaria Ally (16), licha ya kuwa mshindi wa kwanza kutoka Tanzania na kukosha nyoyo za wengi lakini kama isingekuwa juhudi za mwalimu wake huenda asingeyafikia mafanikio hayo.

Fainali hizo ziliandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhi Quraani Tanzania zilifanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Aboubakar Bin Zubeir.

Ushindi wa Ally haukuja kirahisi kama watu wanavyoweza kudhani bali kazi kubwa ilifanyika kuhakikisha anafikia kiwango hicho, kama ambavyo anaeleza mwalimu wake wa kuhifadhisha Quraani, Said Matembe.

Pia Soma

Sio kazi rahisi

Matembe anasema Ally anatokea shule ya msingi ya Ibun Jazar iliyopo Vikindu mkoani Pwani yenye watoto 100 wanaosomea masomo ya dini ya Kiislamu na ndani yake kukiwa na kituoa kinachojighulisha na kuhifadhisha Quraani.

Anasema suala la kuhifadhisha Quraan linahitaji umakini, uvumilivu na moyo wa kujitoa kutokana na ugumu uliopo kuanzia katika ushirikiano na watoto wenyewe.

“Pale kituoni tumeweka taratibu mbalimbali za kuhakikisha mchakato wa kuhifadhisha Quraani unafanyika kwa ufanisi. Kwa mfano tuna taratibu za kuwafadhisha Quraani watoto kuanzia saa sita usiku hadi saa 11 alfajiri. Baada ya hapo wanakwenda kuswali, kisha saa mbili asubuhi wanakutana na walimu wanaowasilikiza walichokihifadhi.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Kitendo cha kuwaamsha saa sita usiku watoto hawakipendi akiwemo Ally ambaye aliona kama namuonea, lakini kumbe tulikuwa tunamjengea msingi mzuri wa mafanikio yake katika safari ya kuhifadhi Quraani,” anasema Matembe.

Anasema katika mchakato huo, Ally kwa nyakati tofauti alionekana ni mzito na mvuvi, lakini yeye akiwa mwalimu na mlezi wake alishagundua kipaji chake ndio maana aliamua kumkazania hadi sasa ameanza kupata mafanikio.

Mbali na hilo, Matembe anasema changamoto nyingine inayowakabili katika mchakato huo ni suala la utandawazi ambapo kituoni kwao wameweka utaratibu wa kutoruhusu watoto kuwa na simu.

“Kwa hali ilivyo sasa ukimkataza mtoto kuwa na simu anaona kama unamzuia asijue mambo yanayoendelea duniani, lakini tunajitahidi kupambana na changamoto hii,” anasema.

Suala lingine ni baadhi ya wazazi kutokuwa mstari wa mbele katika suala la masomo ya dini kwa kuwapa ushirikiano walimu, jambo linalosababisha mchakato wa kuhifadhisha Quraan kutokuwa na ufanisi.

“Mfano mzuri ni wazazi wa Ally, ambao tulipata wakati mgumu kipindi ambacho mtoto huyu alipokuwa akihitaji hati ya kusafiria. Jambo hili lilikwenda kwa kusuasua sana, lakini tulisimama imara hadi akafanikiwa.

“Hivi karibuni kabla ya kushirikia fainali zile (Mei 25), miezi michache Ally alikuwa Kuwait kwenye mashindano ya kimataifa ya kuhifadhisha Quraan yaliyoshirikisha mataifa 80 na alishika nafasi ya 10,” anasema Matembe.

Anasema Ally ni mtoto mwenye kipaji cha kuhifadhi Quraan na hadi kufikia hapo alipitia michujo mitatu kabla ya kutangazwa mshindi wa kitaifa na hatimaye kupata nafasi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye fainali za tuzo za kimataifa za kuhifadha Quraan ambako aliibuka kidedea.

“Alipita michujo miwili ya kanda ya Pwani, kisha akaingia kwenye fainali za kitaifa zilizofanyika Dodoma ambako alishinda na kupewa zawadi ya fedha na tiketi ya kwenda Makkah kwa ajili ya ibada ya Hijja, na hivi karibuni ameahidiwa kupewa kiwanja,” anasema.

Hata hivyo, Matembe anasisitiza hata kama wazazi hawatatoa ushirikiano lakini wao hawawezi kurudi nyuma wala kukata tamaa katika jitihada za kuwasaidia watoto wenye vipaji vya kuhifadhi Quraan.

Ally asimulia

Kwa upande wake Ally ambaye mwakani anaanza kidato cha kwanza anasema malengo yake makubwa ni kuhakikisha anajiendeleza kielimu zaidi na kwamba alikuwa na uhikika wa kushinda kwa namna alivyojiandaa na fainali hizo.

“Ingawa nilikuwa na hofu kutokana na uwezo wa washiriki wenzangu kwa sababu ni wazoefu, wa kimataifa lakini sikujali. Akilini mwangu nilikuwa na wazo la kushinda na siyo kushindwa,” anasema Ally.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwake kufikia hapo kwani ilimchukua miaka miwili kuhifadhi juzuu 30 zilizo katika kitabu hicho kitukufu.

“Nilikuwa mzito, mvivu na mtegaji wa kuhifadhi, kila nilipoambiwa nilihisi mwalimu na wenzake wananionea. Sikujua kumbe ilikuwa ni kwa manufaa yangu na leo hii matunda yameonekana,” anasema.

Ametumia nafasi hiyo, kuwataka vijana wenzake kutokata tamaa ya kusoma masomo ya dini akisema ni njia mojawapo ya kupata mafanikio katika maisha yao iwapo watapata matokeo mazuri.

Akizungumza katika fainali hizo, Majaliwa alitoa wito kwa Waislamu nchini kuwasimamia vyema watoto katika makuzi yao ili waweze kusoma dini hiyo.

Majaliwa anasema, “tuwafunze vijana wetu Quraan vizuri ili waweze kukabiliana na changamoto nyingi zinazoibuka kwenye ulimwengu wa sasa hasa suala la utandawazi na mmonyoko mkubwa wa maadili ulioanza kujitokeza sehemu mbalimbali.”

Chanzo: mwananchi.co.tz