Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa umeme watikisa, waombewa na viongozi 13 wa dini

31395 UMEMEPIC Picha kutoka Ikulu Tanzania

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi 13 wa dini jana walisimama na kuuombea mradi wa umeme utakaozalishwa Mto Rufiji katika bonde la Stiegler ili upate mafanikio.

Maombi hayo ya viongozi wa dini na madhehebu tofauti yalifanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutia saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi huo utakaokuwa ukizalisha megawati 2,115 za umeme utakapokamilika.

Utiaji saini wa mradi huo utakaogharimu Sh6.558 trilioni ulishuhudiwa na Rais John Magufuli pamoja na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly.

“Nataka niwaeleze ukweli, mimi nimekaa kwenye construction industry (sekta ya ujenzi) kama waziri wa ujenzi kwa karibu miaka 20,” alisema Rais Magufuli.

“Nimefanya miradi mingi. Kilomita elfu kwa maelfu, lakini sijawahi kushuhudia katika maisha yangu ya miaka 23, mradi unaosainiwa una viongozi wa dini wengi kiasi hiki.

“Kwa hiyo mradi huu una baraka ya pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haiwezekani watu wote hawa wamejitokeza halafu ushindwe. Halafu wanaoutekeleza wanatoka kule Yesu alikokimbilia.”

Hafla hiyo ilianza kwa maombi na dua, viongozi 13 wa dini walipata nafasi ya kufanya maombi, wakitumia dakika 45 kwa ujumla.

Baadhi ya viongozi wa dini waliopata nafasi ni Sheikh Abubakar Zubeir, ambaye ni mufti wa Tanzania, Askofu Josephat Gwajima (Ufufuo na Uzima), Josephat Gwajima, Nabii Josephat Mwingira (Efatha) na Mchungaji Anthony Lusekelo (Maombezi).

Wengine ni Zainuddin Adamjee (Jumuiya ya Bohora), Askofu Mahimbo Ndolwa (Anglikana), Askofu Gervas Nyaisonga (TEC) na Askofu Polycarp Kardinali Pengo (Jimbo Kuu la Dar es Salaam).

Pia, alikuwepo mwenyekiti wa Hojja Shia; kiongozi wa misikiti ya Ismailia nchini; kiongozi wa misikiti ya Sunni, kiongozi wa waadventista Sabato na mwakilishi wa Kanisa la African Inland.

Katika salamu na maombi yao, viongozi hao walimpongeza Rais Magufuli kwa ujasiri wake wa kutekeleza mradi huo na kuahidi kuendelea kumuombea ili aendelee kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Ulipigwa vita

Rais alisema mradi huo unaojengwa katika pori la akiba la Selous ambalo limo kwenye orodha ya urithi wa dunia, umekuwa ukipigwa vita kwa miaka 40 kwa kisingizio cha uharibifu wa mazingira.

“Kwa hiyo sishangai kama mawazo haya yalikuwa ya Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) tangu mwaka 1970 leo ndiyo tunakuja kuweka saini zaidi ya miaka 40. Nilijua matatizo waliyokuwa wanapambana nayo,” alisema.

“Kila mahali wana sababu. Tulipomega eneo kwa ajili ya utafiti wa uranium walitoa haraka haraka. Tulipotoa eneo la 1.8 per cent kwa ajili ya hydro electric power, tunaambiwa environment (mazingira).”

Alisema mradi huo utatunza mazingira tofauti na baadhi ya wanamazingira wanaodai kuwa utaharibu mazingira.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa kuta mbili kubwa zenye urefu wa mita 1025 na kimo cha mita 131, kujenga bwawa kubwa la kutunza maji lenye urefu wa kilometa 100 na upana kilometa 25 na uwezo wa kubeba mita bilioni 35.2 za ujazo.

Alisema kazi itakayofuata ni mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 235 na baadaye kujenga kituo cha kufua umeme mkubwa.

Alisema eneo la mradi huo ni kilometa 914 za mraba kati ya jumla ya kilometa 50,000 za mraba, huku eneo litakalojengwa mtambo likiwa kilometa 39 za mraba, sawa na asilimia 0.007 ya pori la Selous. Hivyo eneo la mradi litakuwa na asilimia 1.8 la eneo lote.

Akizungumzia mradi huo, Waziri Mkuu wa Misri, Dk Mostafa Madbouly alisema mradi huo utafungua fursa mpya za ushirikiano baina ya nchi yake na Tanzania katika miradi mbalimbali.

Alisema Tanzania na Misri zimekuwa zikishirikiana tangu mwaka 1964 wakati waasisi wa mataifa haya mawili walipoanzisha ushirikiano, wakiunganishwa na Mto Nile.

Alisema mradi huo utazuia ukataji wa miti huku akirejea taarifa ya taarifa ya Tathmini ya Rasilimali ya Misitu (Naforma) ya 2015 inayoonyesha mgawanyo wa aina za matumizi ya nishati na kuni na mkaa zinatumika kwa asilimia 92, petroli asilimia 7 na umeme asilimia moja.

Rais alisema wamebaini kuwa chanzo chake ni cha uhakika, kwa kuwa unatekelezwa kwenye mitandao wa mito iliyopo kwenye maeneo yenye wastani mkubwa wa mvua.

“Kwa tathmini ya awali, mradi huu utazalisha umeme kwa miaka 60 ijayo, Pili gharama za utekelezaji si kubwa ukilinganisha na vyanzo vingine,” alisema.

Alisema bwawa kubwa kuliko yote liko China likizalisha MW22,500 la pili liko nchini Brazil MW14,000, halafu China tena MW13,860.



Chanzo: mwananchi.co.tz