Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Morogoro yafikwa na misiba miwili ya vigogo

33705 CCM+PIC Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Sheikh wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) wilaya ya Morogoro, Abdulrahaman Purusa Kiswabi (55) na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro, Petro Kingu (67) wamefariki dunia kwa nyakati tofauti.

Marehemu Kingu alifariki jana Jumatano, Desemba 26, 2018 majira ya saa 9 usiku katika Hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya presha na kisukari, wakati Sheikh Kiswabi amefariki leo Alhamisi nyumbani kwake maeneo ya Msikiti Mkuu wa mkoa wa Morogoro.

Mtoto wa Kingu, Ivan Kingu akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi amesema baba yake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kujaa maji, kisukari na presha kwa muda mrefu.

Amesema baba yake amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa CCM Morogoro kwa miongo miwili, mwenyekiti wa bodi wa Uwera na kuwa mjumbe wa bodi NTC nafasi aliyokuwa nayo hadi sasa.

Amesema marehemu atazikwa nyumbani kwao Singida kwenye makaburi ya familia ambapo aliwashukuru wana CCM na wananchi wa Morogoro kwa namna walivyojitokeza kumuaga nyumbani kwake Mazimbu.

Akizungumzia kifo cha Sheikh Kiswabi, Katibu Mkuu Mtendaji wa Bakwata wilaya ya Morogoro, Pondo Amani amesema Kiswabi amefariki dunia saa 1 asubuhi ya Desemba 27, kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya tezi dume.

Amani amesema Sheikh Kiswabi ambaye pia alikuwa Imamu mkuu wa msikiti wa mkoa wa Morogoro, amefariki kutokana na maradhi hayo kwa zaidi ya miezi sita na ameacha wajane wawili na watoto wanane kwa wanawake wote wawili.

“Mazishi ya Sheikh Kiswabi yatafanyika kesho Ijumaa baada ya swala ya Ijumaa na atazikwa kwenye makaburi ya familia yaliyopo kijiji cha Lukangazi kata ya Mikese Morogoro Vijijini.”alisena Amani.

Amani amesema kwa mujibu wa katiba ya Bakwata wilaya, nafasi yake inakaimishwa kwa muda wa siku 90 na Sheikh mwingine atakayeteuliwa na baada ya muda huo, Bakwata Taifa itateua Sheikh wa wilaya hiyo.

Amesema Bakwata wilaya, msikiti mkuu wa Boma Road na Bakwata mkoa utasimamia shughuli zote za mazishi na maandalizi baada ya kukaa kikao cha pamoja leo.



Chanzo: mwananchi.co.tz