Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgomo wa daladala Moshi waingia siku ya pili

30078 Pic+mgomo Mgomo wa Daladala Moshi

Tue, 4 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Leo ni siku ya pili tangu  kuanza kwa mgomo wa daladala mjini Moshi jambo linalowalazimu baadhi ya wananchi kutumia nguvu ya ziada kupata usafiri wa kwenda na kurudi kazini, shuleni na katika majukumu yao mengine ya kila siku.

Wapo wanaokodi bodaboda, Bajaj, kutembea kwa miguu na wengine kutumia taksi.

Mgomo huo ulioanza jana umetokana na madereva wa daladala kusitisha kutoa usafiri wakipinga Bajaj kupakia abiria katika vituo vya mabasi.

Daladala ambazo hazitoi huduma tangu jana ni zile zinazotoa huduma ya usafiri kati ya Moshi mjini na KCMC, Majengo, Soweto na Pasua.

Wakizungumzia adha hiyo, baadhi ya wakazi wa mjini Moshi wamesema mgomo huo umeleta athari zaidi kwa wafanyakazi, wafanyabiashara, wanafunzi na wananchi wa kawaida.

Jackline Mroso, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majengo amesema kutokana na mgomo huo imemlazimu kutembea umbali mrefu kutafuta usafiri wa daladala ili aweze kufika shule kwa wakati.

"Yaani niliamka asubuhi na mapema niwahi shule lakini nilikaa kituoni zaidi ya saa mbili bila mafanikio. Kilichoniokoa alikuja msamaria mwema akanipa lifti,” amesema Jackline.

Mfanyabiashara wa eneo la Msaranga, Agatha Joseph ameeleza kushindwa kwenda sokoni kununua bidhaa kutokana na mgomo huo.

"Tumezoea kuamka saa 11:00 asubuhi kwenda Mbuyuni kununua vitu magengeni lakini jana na leo tumeshindwa kwa sababu ukipanda bodaboda ni gharama kubwa. Tunaomba viongozi wetu walitazame hili jambo kwa umakini,” amesema Agatha.

Kiongozi wa daladala zinazofanya safari kati ya Moshi mjini na KCMC, Ibrahim Mzava amesema jana mchana walipokutana na  uongozi wa Manispaa ya Moshi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), walikubaliana kuziondoa Bajaj hizo lakini hakuna kilichotekelezwa hadi leo.

"Walitueleza kuwa watatangaza kuziondoa Bajaj hizo lakini hadi leo asubuhi hakuna kinachoendelea. Tulichoamua ni kupaki daladala  zetu hadi kieleweke,” amesema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alipoulizwa kutotekelezwa kwa makubaliano ya wenye daladala na Sumatra amesema atafanya kikao na madereva wa Bajaj ili kuwapa maelekezo ya namna ya kufuata sheria za utoaji wa huduma kulingana na leseni inavyotaka.

Soma zaidi: Mgomo wa daladala watikisa Morogoro, Moshi



Chanzo: mwananchi.co.tz