Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchungaji aeleza alichosema mwandishi wa habari kabla ya kufariki

33291 Pic+mchungaji Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mchungaji Sesilia Makundi ameeleza neno la mwisho alilotamka mwandishi wa habari wa Efatha, Ikupa Ngao siku chache kabla ya kifo chake.

Ikupa alifariki dunia Desemba 20, 2018 katika Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 24, 2018 wakati akitoa salamu za rambirambi wakati wa ibada ya kuaga mwili, Mchungaji Makundi alisema wakati anafika hospitalini hapo marehemu alimuambia ‘asiwe na wasiwasi amepona.’

“Ilikuwa asubuhi ya tarehe 10 wakati naenda kumchukulia mtoto wangu dawa nilikuta Ikupa ndio anafikishwa hospitalini akiwa mahututi, alikuwa mzima na alikubali tufanye sala ya utakaso baada ya sala neno lake la mwisho lilikuwa ‘kwa maombi haya nimepona,” amesema mchungaji huyo.

Katika msiba huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa wilaya ya  Arumeru, Jerry Muro, waombolezaji walieleza jinsi marehemu alivyokuwa mcheshi na mpenda watu.

Muro ambaye aliwahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari amesema marehemu ameacha pengo kwa familia na tasnia ya habari kwa ujumla.

“Kwa umri wake amefanya kazi kubwa sana, kwa hiyo kufa na umri mdogo si tatizo, tatizo ni je umefanya nini maana unaweza kuwa na miaka 50 usifanye chochote,” amesema Muro.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco) mshauri wa wanafunzi, Dr Hoyce Mbowe amesema Ikupa alikuwa mwanafunzi mwaminifu na mwenye bidii.

“Alikuwa rafiki wa walimu, wanafunzi wenzake hakubagua mtu alikuwa mcheshi muda wote, tutamkumbuka daima,” amesema.

Ikupa ambaye pia ni mwanafunzi wa Tudarco mwaka wa pili akisomea uandishi na mawasiliano ya umma alizaliwa mwaka 1980 mkoani Iringa na baada ya kuagwa mwili wake ulizikwa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam

Enzi za uhai  aliwahi kufanya kazi kituo cha redio cha Praise Power, Wapo Redio na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti.



Chanzo: mwananchi.co.tz