Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Elizabeth Ng’unga (36) ameuawa kikatili kwa kutobolewa macho katika eneo la Ilula, wilayani Kilolo mkoani hapa, mumewe Aron Mkumbo amesimulia.
Mkumbo amesema licha ya kutobolewa macho, ameshuhudia mwili wa mkewe ukiwa umefungwa kwa kamba ya manila shingoni huku mkono wake mmoja ukiwa umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mchungaji Elizebeth anadaiwa kuuawa katika mlima wa Uhambingeto, Ilula wilayani Kilolo alikokuwa ameenda kwa shughuli za kifamilia.
Awali, mwili wake ulizikwa katika eneo la mauaji baada ya kuonekana kuharibika vibaya na ndugu zake kutopatikana, lakini baadaye ililazimika kuukua ili uzikwe upya katika Kijiji cha Ilambilole.
Katika taarifa yake jana, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile ametangaza kuuawa kwa mchungaji wa kanisa hilo ambaye pia alikuwa akifanya kazi kwenye ofisi yake.
“Nasikitika kutangaza kifo cha Mchungaji Elizabeth, alijeruhiwa na watu wasiojulikana akiwa kwenye shughuli zake za kifamilia. Kutokana na mwili wake kuharibika, mazishi yamefanyika Jumamosi (jana),” alisema Askofu Gavile.
Akisimulia tukio hilo huku machozi yakimtoka, Mkumbo alisema wiki moja iliyopita mke wake alisafiri kwenda kusimamisha shughuli za shamba katika vijiji vya Makungu na Ukwega.
Alisema awali baada ya mkewe kuondoka kulikuwa na mawasiliano mazuri baina yao lakini yalikatika ghafla Jumatano asubuhi siku anayodaiwa kuuawa.
“Jumatano asubuhi tuliwasiliana japo kule alikokuwa kulikuwa na shida ya mtandao, akaniambia amepakia mzigo (kutoka shamba) kwenye gari hivyo natakiwa kuopokea. Alipakia ndizi, parachini, viazi na maharage,” alisema Mkumbo.
Alisema aliyemtumia ujumbe kwenye simu yake kuwa vitu hivyo vimeshapakiwa kwenye gari ni shemeji yake ambaye anaitwa Naftari, hivyo alienda kupokea bila wasiwasi.
Mkumbo alisema baada ya kupokea mzigo huo na kurejea nyumbani, hakuweza tena kumpata mkewe kwenye simu licha ya kupiga simu mara nyingi.
“Siku ya Jumatano nilipiga sana simu bila mafanikio, nilianza kupata wasiwasi lakini nikalala. Alhamisi nikaendela kumtafuta, hata hivyo nilijua huko aliko hakuna mawasiliano. Niliwapigia watu wa karibu ila walionyesha kama alishaondoka,” alisema.
Mkumbo alisimulia kuwa usiku wa kuamkia Ijumaa, alipigiwa simu na mtu asiyemjua akijitambulisha kama shemeji yake kwa maana ya dada wa mkewe.
“Nakumbuka ilikuwa saa sita usiku, simu iliita nikapokea na akajitambulisha. Aliniuliza ikiwa mke wangu yupo nyumbani nikasema hayupo alisafiri lakini simpati,” alisema Mkumbo.
“Yule mtu alikata simu. Ikabidi niwapigie viongozi wa kanisa kuwaeleza jambo hilo. Saa 11 alfajiri (huyo mtu) alipiga simu tena, safari hii akasema mke wangu amefariki na mwili wake umeshazikwa.”
Alisema ilibidi amtafute shemeji yake anayeitwa Naftari ambaye dakika ya mwisho alimtumia ujumbe kuhusu mzigo alipowasiliana na mkewe, lakini alisema waliachana tangu Jumatano.
Mkumbo alisema Naftari alisema waliachana na Mchungaji Elizabeth baada ya kupata mteja wa kununua mahindi na alizeti waliyokuwa wamevuna.
“Kama kweli aliuza mahindi basi alikuwa na kama milioni mbili, hata hivyo sijui ukweli wowote kuhusu hilo,” alisema Mkumbo.
Alisema kutokana na utata huo, aliongozana na baadhi ya viongozi wa KKKT, Iringa mpaka polisi ambako walitoa taarifa wakiomba mawasiliano yake yafuatiliwe ili kujua aliko mkewe kwa sababu hakuwa anaamini taarifa za kuuawa kwake.
Alisema Jumamosi asubuhi, alishauriwa kwenda Kituo cha Polisi Ilula ambako alipata taarifa za kuuawa kwa mwanamke ambaye tayari alikuwa amezikwa kutokana na mwili wake kuharibika. “Nilienda mpaka makaburini nikaona kaburi jipya na kwa sababu watu walikuwa wamejaa, nilisimama pembeni huku shughuli ya kufukua mwili ikiendelea,” alisema.
Alisema baada ya mwili kufukuliwa na kuwekwa kwenye machela, aliona kitambaa cha mkewe hapo nguvu zikamwishia kwa sababu alianza kuamini taarifa za kuuawa kwake.
Alisema kwa sababu polisi kwa wakati huo walikuwa wakimuhoji na msingamano wa watu, hakuweza kusogea kwenye mwili, badala yake ilipigwa picha ya usoni na kuletwa athibitishe.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Alan Bukumbi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, polisi wanaendelea kufanya uchunguzi.