Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbuzi 2,000 kuchinjwa sherehe za Eid

13064 Mbuzi+pic TanzaniaWeb

Tue, 21 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Waislamu duniani wakisherehekea sikukuu ya Idd el Hajj, Taasisi ya African Relief Organization (Aro) itachinja zaidi ya mbuzi 2,000 na ng’ombe 10 kwa ajili ya msaada kwa vituo vya watoto yatima, misikiti, familia zisizo na uwezo na taasisi nyingine zenye uhitaji.

Kitoweo hicho kitagawiwa katika mikoa 12 nchini ikiwamo Dar es Salaam ambako ng’ombe 10 na mbuzi 800 watachinjwa leo Agosti 21 katika kijiji cha Gezaulole, Wilaya ya Kigamboni.

Akizungumzia shughuli hiyo, ofisa uhusiano wa Aro, Jamal Lwambow amesema taasisi hiyo inayotekeleza miradi mbalimbali nchini, imekuwa na utaratibu wa kugawa nyama  kipindi cha sikukuu ya Idd el Hajj kama sadaka kwa makundi ya watu wasiojiweza.

“Taasisi hii inamilikiwa na watu wa Kuwait na kinapofika kipindi kama hiki, wanatoa msaada kwa watoto yatima, familia maskini na taasisi nyingine zenye uhitaji. Mwaka huu tunachinja zaidi ya mbuzi 2,000 katika mikoa 12 nchini,” amesema huyo.

Mkuu wa malezi wa Aro, Ibrahim Yousef amesema taasisi hiyo inaendesha zoezi la uchinjaji katika maeneo mengine ya Tanga, Arusha, Moshi, Lindi, Mtwara, Tabora, Dodoma, Singida, Rufiji, Morogoro, Iringa na Zanzibar.

Naye mkazi wa Gezaulole, Iddi Shaaban ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada walioutoa kwao na kuwataka wengine wenye uwezo wajitoe katika kusaidia kaya maskini kwa kuwa watajiwekea akiba mbinguni.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz