Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbali na kufanya tendo la ndoa kuondoa janga la Mv Nyerere, Wakara wanaabudu miungu kibao

20618 Ukara+pic TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kwa Wakristo na Waislam, Mungu ni mmoja akiwa na mitume na manabii wanaotumika kufikisha ujumbe kwa waumini.

Hii ni tofauti na waumini wa dini na madhehebu ya asili ambao wana mawasiliano moja kwa moja na miungu tofauti wanayoiabudu kulingana na maeneo, kabila na matukio yaliyowakuta.

Wakati kukiwa na hofu kwa wakazi wa Ukara wilayani Ukerewe kuingia katika mila ya kufanya mapenzi kwa lengo la kujitakasa baada ya kufiwa na wenzi wao, kisiwa hicho pia kinaendeleza mila ya kuamini miungu ya jadi na baadhi ya wakazi wake wana dini, madhehebu na ibada za asili.

Jana tuliona jinsi mila hiyo inavyowaweka hatarini baadhi ya wakazi wa Ukara waliopoteza waume au wake zao katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere ambayo ilisababisha vifo vya watu wapataw 230, wengi wakiwa wanatoka gulioni katika kisiwa jirani.

Wafiwa hao wanatarajiwa kutengwa hadi hapo watakapotakaswa kwa kufanya mapenzi na mtu kutoka ukoo, eneo au kisiwa kingine ndipo warudi kujumuika na wenzao, mila ambayo inaweza kuwaingiza katika magonjwa hatari ya kuambukiza, hasa Ukimwi.

Athari kama hizo zinaweza kuwepo katika imani.

Kisiwa hicho chenye wakazi zaidi ya 50,000 kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo, Cornel Maghembe, kinakadiriwa kuwa na zaidi ya miungu 16 kulingana na familia, koo na maeneo yao.

Karibu kila kijiji kati ya vinane vilivyo katika kata nne, kina mungu zaidi ya mmoja.

Kwa hesabu ya idadi ya watu na miungu inayopatikana katika kisiwa cha Ukara, inakadiriwa kila kundi la zaidi ya watu 3, 000 kisiwani humo lina mungu wao.

“Miungu yote ina nguvu na inatenda kulingana na maombi,” alisema Zakaria Chibuga, mmoja wa wazee wazawa wa Ukara alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu.

Chibuga anasema wakazi wa eneo la Bukungu huamini mungu aitwaye Nyang’wena, ambaye wanaamini kuwa anaweza kugeuza majani ya miti kuwa mamba.

Kisu kuchana makalio

Chibuga alisema mungu mwingine anayeabudiwa na wakazi wa Nyamalulu anaitwa Imbandam ambaye wakazi wanamuamini kuwa ana uwezo wa kubaini wasiokiri makosa yao.

Lakini njia ya kumtumia mungu huyo kupata mkosaji ni ile ya wanajamii kupakwa dawa na kupitisha makalio yao kwenye kisu bila ya kuvaa nguo.

“Asiyehusika atatoka salama lakini mkosaji hukatwa na hivyo kufichua uovu wake mbele ya umma,” anasema Chibuga.

Kijiji cha Nyamanga pia kina mungu wao aitwaye nyablebeka ambaye ni jiwe wakati kijiji cha Nyamanga kina miungu watatu ambao ni nyafunano, avanga na abamulela na miungu wa kisiwa cha Kome ni watatu, akiwemo nyatesho.

Nyafunano na abamulela ni ng’ombe wanaoishi kwa kurandaranda mitaani bila kula mazao wala kuaharibu mali za wanakijiji. Wakazi wakitaka kula nyama zao, huwaua kwa kuwapiga na fimbo na mikuki hadi kufa na nyama yote huliwa kwa siku moja.

Mkazi mwingine wa Ukara, Emily Masyenene aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa nyateso huibuka na aina mbalimbali ya vyakula kama ndizi, mihogo na viazi.

“Baada ya muda maalumu, nyateso hupotea na kurejea ndani ya maji,” alisema Masyenene

Miungu wengine wa Kome ni chame na luliba ambaye ni mawe mawili ambayo huaminika kuwa yanaweza kugeuza maharusi kuwa mawe pia.

Soma Zaidi:

Hofu yatanda wakazi Ukara kufanya tendo la ndoa kuondoa janga la Mv Nyerere

 

Ajali ya Mv Nyerere na ‘hasira’ ya miungu

Hata ajabu ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018, inahusishwa na hasira za mungu kama wanavyoamini wenyeji wa kijiji cha Bwisya kulikotokea ajali hiyo.

“Halisemwi hadharani, lakini wenyeji wanahusisha ajali hii na kitendo cha kuuzwa kwa eneo maalumu la ibada la Mubyalo ambako ndiko yalikuwa makazi ya mungu aitwaye nyamugwe,” alisema Chibuga

Chibuga alisema eneo hilo ambalo sasa limekuwa makazi liliuzwa kwa mchungaji wa moja ya makanisa ya uamsho ili kujenga kanisa kabla ya kubadilishwa na kuwa makazi.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz