Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawaidha ya Ijumaa: Sababu ya kuumbwa kwa mwanadamu

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lengo la kuumbwa ulimwengu?

Ulimwengu ambao ni dunia yetu na vyote vilivyoko angani katika sayari na galaksi viliumbwa na Mungu kwa lengo maalum. Qur’an inatueleza juu ya hili pale Mwenyezi Mungu aliposema;

“Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyomo katikati tukicheza. Hatukuviumba isipokuwa kwa haki lakini watu wengi hawajui” (Qur’an 44:38).

Kwa hiyo ulimwengu haukuumbwa kimchezomchezo tu isipokuwa kuna lengo kuu na tukufu la kuumbwa kwake. Uwepo wa ulimwengu ikiwa ni pamoja na dunia yetu ni kwa ajili ya haki.

Haki yenyewe ni mwanadamu kumuabudiwa Muumba wa mbingu na ardhi kama walivyofundisha mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu kuanzia Adam hadi mtume Muhammad.

Mienendo ya sayari, jua, mwezi na kila kilichoko angani, uwepo wa maji katika dunia mimea, wanyama, wadudu, upepo na hewa ni maandalizi ya kumwekea mwanadamu mazingira ya kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Uislamu, kuumbwa kwa ulimwengu ni matokeo ya sifa ya uumbaji aliyonayo Mwenyezi Mungu na umekuweko tangu uumbwe kwa utashi wake.

Viumbe vyote vilivyoko ulimwenguni, akiwemo mwanadamu, viko hapa kwa utashi na mpango wake. Hebu tuangalie Uislamu unasema nini kuhusu mwanadamu na lengo la kuumbwa kwake.

Kuumbwa kwa mwanadamu.

Dini mbalimbali zimeelezea jinsi mwanadamu alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu. Uislamu nao umeelezea kuumbika kwa mwanadamu. Kwanza, Uislamu unamuelezea mwanadamu kama kiumbe aliyeumbwa baada ya kuumbwa viumbe wengine wengi kabla yake kama vile malaika, majini, wanyama na mimea.

Qur’an inasema “Je haukumpitikia mwanadamu muda mrefu hakuwa kitu chenye kutajika?” (76:1).

Pili, Uislamu unaelezea maada ya asili iliyotumika kumuumba mwanadamu kwamba ni udongo. Qur’an inasema “Na aliposema Mola wako kuwaambia malaika hakika mimi nitaumba mtu kutokamana na udongo wa mfinyanzi utoao sauti uliovunda” (15:28).

Kwa hiyo asili ya mwanadamu ni udongo na hili limeelezewa na dini zote kuu tatu ulimwengu yaani Uislamu, Ukristo na Uyahudi.

Lakini Uislamu ukaendelea kuelezea mbali ya maada mwanadamu ni kiumbe wa kiroho pia. Baada ya kuwaeleza malaika kuwa anataka kumuumba mtu, Mwenyei Mungu alisema.

“Na nitakapomsawazisha sura na kupulizia ndani yake roho itokanayo na mimi hapo angukeni chini mumsujudie” (Qur’an 15:29).

Hapa tunafahamishwa kwamba kupuliziwa roho itokayo na Mwenyezi Mungu ndiyo hatua ya pili ya uumbaji wa mwanadamu. Kwanza ni umbile tu lililotokana na udongo lisilo na uhai.

Mara baada ya kupuliziwa roho ndipo akawa mtu kamili. Maana yake ni kwamba bila roho mwanadamu ni umbile mfu lisilo na chembe ya uhai. Kati ya mwili na roho kilicho muhimu zaidi ni roho.

Hii ni kwa sababu roho ndiyo nguvu impayo mwanadamu uhai akawa na jeuri ya kufanya yale ayafanyao kama vile hakuumbwa na roho inapotolewa mwanadamu hupoteza uhai wake na kuitwa maiti.

Katika aya hiyo hapo juu, tunaona Mwenyezi Mungu akiwaambia malaika wamsujudie mtu wa kwanza kuumbwa mbaye ni Adam.

Hapa tunaweza kuuliza, Uislamu unakataza kiumbe kumsujudia kiumbe mwingine mbona hapa Mwenyezi Mungu anawaamrisha malaika wake wamsujudie Adam?

Jibu la swali hili ni kwamba, katika Uislamu kuna kusujudu kwa nia ya ibada na kusujudu kwa nia ya heshima. Malaika walimsujudia Adam kusujudu kwa heshima tu na siyo ibada.

Hatua ya tatu ya uumbaji wa mwanadamu ni pale anapoumbwa ndani ya mji wa mimba wa mama yake. Uislamu unaielezea hatua hii kwa kutufahamisha kwamba mwanadamu ameumbwa kwa maji yaitwayo manii.

“Na mwanadamu atazame ameumbika kwa kitu gani? Ameumbika kwa maji yatokayo kwa kuchupa kwa nguvu kutoka kati ya mfupa wa kifua na uti wa mgongo” (Qur’an 86:5-7).

Katika aya nyingine Mwenyezi Mungu akasema “Je hatukukuumbeni kutokamana na maji madhalili. Basi tukayaeka katika mahali madhubuti. Kwa kiwango na muda maalumu? Na tukakadiria na sisi ni wabora wa kukadiria” (Qur’an 77:20-23).

Naam, hiyo ndiyo asili yetu pamoja na ujanja, majivuno na kiburi tulichonacho mara tufikapo duniani na tukaona tunajiweza.

Mwenyezi Mungu anayetujua anasema. “Hakika mwanadamu ni mwenye kuasi, pale anapojiona amejitosheleza”. Tumefahamishwa yote haya kuanzia kuumbwa kwa ulimwengu na kuumbika kwetu ili tutafakari.

Maendeleo makubwa yaliyofikiwa na mwanadamu katika sayansi, teknolojia, habari na mawasiliano yamewafanya wanadamu wengi kujiona wamejitosheleza na hivyo kupunguza imani yao kwa Mwenyezi Mungu na hata kumkana au kumsahau kabisa.

Mwenyezi Mungu anauliza akisema “Je hivi waliumbika kutokamana na kisicho kitu au wao ndio waumbaji? Au ni wao walioziumba mbingu na ardhi? Lakini hawana yakini” (Qur’an 52:35-36).

Hakika katika maumbile mbali mbali aliyoumba Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini na hata katika mwanadamu mwenyewe kuna dalili kadha wa kadha za kuthibitisha uwepo wake.

Ulimwengu na viumbe vilivyomo ndani yake haviko hapa kwa bahati mbaya ua chance creation kama wanavyodai wanaopinga uwepo wa Mwenyezi Mungu.

Toleo lijalo tutaangalia dalili za uwepo wa Mwenyezi Mungu katika kuumbika kwa mwanadamu hatua kwa hatua kwa mujibu wa Uislamu.



Chanzo: mwananchi.co.tz