Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka tena! Waumini waapa kumlinda Askofu KKKT

Wauminipic Data Edward Mwaikali,

Tue, 29 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mambo bado na mgogoro unazidi kuchukua sura mpya. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na kile kinachoendelea ndani ya Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde baada ya mkutano kuitishwa na kupiga kura kumng’oa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo, Edward Mwaikali, vijana wameibuka na kuapa kumlinda.

Hatua hiyo inakuja wakati leo maaskofu wa kanisa hilo wakikutana jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine mgogoro huo unatarajiwa kujadiliwa.

Awali, kulizuka mgogoro kutokana na hatua ya Askofu Mwaikali kuyahamisha makao makuu ya dayosisi hiyo kutoka Tukuyu kwenda Ruanda jijini Mbeya, jambo ambalo lilizusha mvutano mkali.

Akisoma nakala ya tamko la vijana wakati wa ibada iliyofanyika Usharika wa Ruanda jijini Mbeya jana, Katibu wa Kwaya ya Dayosisi ya Konde, Michael Mahenge alisema hawakubaliani na uamuzi wa Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Frederick Shoo na kuanzia sasa watalinda mali za kanisa na viongozi wao kwa gharama zozote.

“Tunapinga uamuzi wa Askofu Shoo kwani alipaswa atumie busara kwa kukaa na viongozi wa pande zote mbili kukubaliana sio kumuondoa Askofu Mwaikali na Mkuu wa Jimbo la Mbeya Magharibi, Mchungaji (Nyibuko) Mwambola. Sisi tunawatambua kuwa ni viongozi halali.

Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mbeya Mashariki na Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Nyibuko Mwambola alisema chanzo cha mgogoro ni shinikizo la kuuzwa kwa mali za kanisa zilizopo eneo la Matema wilayani Kyela.

Advertisement Akizungumza jana wakati wa ibada, Mwambola alisema tatizo sio kugombea kiti kama inavyoelezwa bali ni mali za kanisa likiwemo eneo lenye miradi ya hospitali, chuo, eneo la wazi na nyumba ya wageni vilivyopo Matema.

“Tukiwa viongozi wa Konde msimamo wetu ni kuwa mali hizo hazitauzwa kulipa mkopo,’’ alisema Mwambola bila kuweka wazi mkopo huo.

Pia, alikosoa uamuzi wa mkutano uliomwondoa Askofu Mwaikali na wakuu wa majimbo ya Mbeya Mashariki na Magharibi akisema haukufuata utaratibu wala Katiba ya KKKT.

“Leo Askofu Mwaikali alitaka kuja hapa ibadani kuzungumza nanyi, lakini nimemuomba apumzishe akili kutokana na hali ilivyo kwa sasa ila kikubwa tuendelee kumuombea na Mungu asimame naye katika mgogoro huu,’’ alisema.

Katika hatua nyingine, Mwambola alisema Machi 26, 2022 wamepokea barua za kufungwa kwa akaunti zote za majimbo ya Dayosisi ya Konde ili washindwe kujiendesha ikiwemo kulipa wafanyakazi akisema sio kitu sahihi.

“Jana asubuhi tumeletewa barua ya akaunti za majimbo yote kufungwa ila tunaishukuru benki moja (inahifadhiwa) haijakubaliana na hilo hivyo, wamejiweka kando na mgogoro,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa kinachoendelea kwa sasa walitegemea Dk Shoo angetafuta suluhu ya mgogoro huo lakini, kwa kufunga akaunti ni kama anachochea hivyo watachukua uamuzi mgumu.

Habari za kuaminika ambazo Mwananchi limezipata na ambazo hakuna aliyetaka kuthibitisha ni kwamba, viongozi hao wameanza kukusanya fedha ili kufungua kesi mahakamani.

“Kuna taratibu tumeanza kuchukua na Katibu Mkuu wa Dayosisi kwa sababu katika Katiba yetu hatuna sehemu inampa jukumu Askofu Mkuu kuwaondoa viongozi na kufunga akaunti za kanisa,” alisema.

Askofu KKKT ang’olewa Konde, yeye agoma

Chanzo: www.tanzaniaweb.live