Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maombi, mikesha vyatawala kuombea uchaguzi

F69aa2fe485fcccf023f48e9435857f0 Maombi, mikesha vyatawala kuombea uchaguzi

Sun, 25 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NYUMBA mbalimbali za ibada zimeendelea kufanya maombi, yanayokwenda sambamba na mikesha kuomba amani na utulivu katika uchaguzi mkuu, utakaofanyika baada ya siku tatu kuanzia leo.

Aidha, viongozi wa serikali wa ngazi tofauti na wa dini, wameendelea kukemea na kusihi Watanzania na wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa, kumalizia kampeni kwa amani na kupiga kura bila vurugu taifa liendelee kuwa mahali salama pa kuishi.

Miongoni mwa nyumba za ibada ambazo gazeti hili limebaini ibada kuendelea ni pamoja na Kituo cha Ufuasi na Uenezaji wa Injili cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam cha Agape, kilichopo Mbezi Kibanda, kilichofanya mkesha mkubwa juzi uliohusisha maombi maalum kwa taifa ili uchaguzi ufanyike kwa amani.

Waumini wa Kanisa la Elightened Christian Gathering (ECG) la jijini Dar es Salaam, pia walifanya maombi maalumu ya kuliombea taifa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28.

Maombi hayo yaliyoongozwa na Mwangalizi wa Makanisa yote ya ECG nchini, Mtume Mtalemwa Dionis na ujumbe mkubwa ulikuwa ni namna gani Watanzania wanapaswa kuitunza na kuilinda amani iliyopo nchini hususani kipindi hiki cha uchaguzi.

Aidha, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kibwegere lililopo eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, lilianza maombi Jumatatu kuanzia saa 12 jioni kila siku kuombea uchaguzi mkuu na juzi (Ijumaa) kulikuwa na mkesha kwa ajili hiyo.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Huduma ya World Ministries, Damas Thadey aliwataka viongozi wenzake wa dini kuheshimu madhahabu kwa kutoruhusu nyumba za ibada, kutumiwa na wagombea kufanya kampeni, kwa kuwa nyumba hizo zipo kwa kuduma za kiroho na kimwili na si kwa ajili ya itikadi za kisiasa.

Aidha, jana katika mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dodoma, viongozi wa dini walisisitiza wananchi watakaopiga kura wakishamaliza, warejee nyumbani kupumzika na wasizagae mitaani ili kuzuia uvunjifu wa amani kutokea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dodoma, Shehe Mustafa Shaban, alisema viongozi wa dini hivi karibuni baadhi walipotoka kwa kunadi sera, kutangaza wagombea na kushabikia vyama vya siasa kazi ambayo si wajibu wao .

Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelpia Assembly of God, Dk Yohana Masinga, alisema taifa limempa nafasi Mungu na kiongozi wake (Rais John Magufuli) akaamua kumpa Mungu nafasi wakati wa corona, hivyo viongozi wa dini wanatakiwa kuomba uchaguzi upite kwa amani.

Mjumbe wa Baraza la Mashehe Mkoa wa Dodoma, Shehe Kisusu Mvumbo alisema amani inatakiwa kutamalaki nchini kwa kuhakikisha kwamba wao kama viongozi wa dini wanaombea uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu.

Akifungua mkutano huo wa viongozi wa dini, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge aliwataka kutumia nafasi zao kuhubiri amani na utulivu .

Kutoka mkoani Shinyanga, Mkuu wa Mkoa huo, Zainabu Telack aliwaambia wananchi kuwa siku ya kupiga kura amani na utulivu vitatawala, hivyo wenye sifa wajitokeze kwenda kupiga kura na kurudi nyumbani kwenda kusubiria matokeo kwa utulivu.

Jumuiya ya Viongozi Wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wamelaani tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutoa lugha za vitisho jambo linaloweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu.

Mratibu wa Jumuiya, Saumu Rashid alisema kumekuwapo na lugha za vitisho zinazotolewa na baadhi ya viongozi, jambo alilosema linaweza kuhatarisha amani iliyopo.

Mkoani Mbeya, Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila alipokutana na vikundi mbalimbali vya waimbaji wa nyimbo za dini za Kikristo na Kiislamu kwenye ukumbi wa Mkapa mkoani humo, aliwataka kutunga na kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kuhimiza amani.

Huko mkoani Kigoma viongozi wa dini wamewataka wagombea, viongozi wa vyama vya siana na wanachama wao kufuata taratibu za kukata rufaa wasiporidhika na matokeo ya uchaguzi badala ya kufanya vurugu zinazoweza kuvuruga amani na usalama wa nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz