Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania mazishi ya mke wa AG

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasili kata ya Luchelele Wilaya ya Nyamagama mkoani Mwanza mkoani kuongoza ujumbe wa Serikali katika ibada ya mazishi ya Natalia Kilangi.

Natalia ambaye ni mke wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Professa Adelardus Kilangi alifariki Jumamosi iliyopita ya Agosti 3, 2019 saa 7 mchana katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alipokuwa akiendelea na matibabu ya ugonjwa wa kiharusi.

Viongozi mbalimbali wamejitokeza leo Jumatano Agosti 7,2019 katika ibada hiyo inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala.

Akisoma wasifu wa Natalia, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dotto Bulendu amesema marehemu alifariki kwa ugonjwa wa kiharusi.

"Marehemu alikuwa mhadhiri wa Saut kitivo cha sayansi ya jamii. Ameacha watoto watatu na mume mmoja," amesema Bulendu

Baadhi ya viongozi wa kisiasa na kiserikali waliohudhuria ibada hiyo ni; Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mtungi na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally.

Pia Soma

Akizungumza katika ibada hiyo, Dk Bashiru amesema kifo cha Natalia ni pengo kubwa katika taaluma.

"Tumepoteza shujaa katika uwanja wa taaluma, amepotea katika kipindi ambacho Taifa linahitaji wanataaluma, ombi langu tuendelee kumuombea,” amesema Dk Bashiru

Naye Spika Ndugai amesema marehemu amemuacha mumewe katika mazingira magumu kulingana na shughuli zake hivyo kutaka aombewe.

"Tumkumbuke katika sala zetu, Profesa Kilangi, anafanya kazi nzito sana ambazo zinahitaji kusaidiwa na mama (mke) hivyo kuondokewa na mama katika mazingira haya lazima uwe mtihani," amesema Spika Ndugai

Kaimu Sheikh wa mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi amesema, "Ni tukio kubwa na msiba mkubwa,  Mungu awape amani katika kipindi hiki kigumu.”

Chanzo: mwananchi.co.tz