Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahubiri ya Jumapili; Kwaresima iguse maisha yetu

50898 Pic+kwaresma

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naitwa Mchungaji Christosiler Kalata kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Nikukaribishe katika Jumapili hii njema katika kipindi hiki ambacho tunatafakari mateso yake Bwana wetu Yesu Kristo.

Leo nakuletea neno la Mungu ambalo peke yake linaweza kubadilisha maisha yako na kuanza kuishi maisha ya toba na kurejea katika upendo wa Mungu.

Neno ambalo litakuongoza kutembea katika ujumbe wetu wiki hii ni la Kwaresima na linatoka katika Biblia kitabu cha 1 Wakorintho 15:14 linasema “ Tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. ”

Kwaresima ni kipindi ambacho Wakristo wengi wanaingia katika mfungo kuelekea Pasaka kipindi ambacho Yesu Kristo alikufa msalabani na siku ya tatu alifufuka kutoka kwa wafu.

Mfungo huu unaweza kuchukua siku arobaini au hata na zaidi.

Kipindi hiki kinaanza na ibada ya siku ya Jumatano ya Majivu ikiwa ni ishara ya kutubu na kurejea kwa Mungu na huu ni wakati wa mkristo kuwa mnyenyekevu na kujiona kwamba amemkosea Mungu kwa matendo yale yasiyompendeza.

Kipindi cha Kwaresima kinatukumbusha waumini wote juu ya kufa na kufufuka kwake Yesu Kristo na ufufuko ndio msingi hasa wa imani yetu sisi Wakristo.

Kipindi hiki cha Kwaresima kinatukumbusha na kuendelea kukaa tukitii maongozi ya Mungu.

Tendo la kufunga yaani kubadili tabia ya ulaji kiasi cha chakula kwa siku, hata aina ya chakula ni kitu ambacho kinamjenga mtu.

Kufunga si katika kufunga chakula peke yake, bali kuzuia hata matamshi ya maneno yetu yanayokwaza wengine na hiki ni kipindi cha kuishi vema na majirani zetu.

Ni kipindi cha kufanya matendo yanayowajali wengine, kukaa katika neno la Mungu, kufanya kazi kwa bidii, kuboresha hali ya maisha yetu, kutii viongozi wanaotuongoza, na kuwaombea kwa Mungu.

Bwana wetu Yesu Kristo amekuja ili tuwe na uzima kisha tuwe nao tele.

Tunapokuwa hatuna uzima huu sio mapenzi ya Mungu ambayo ameyakusudia katika maisha yetu, kushiriki njia ya msalaba maana yake ni kukaa katika baraka za Mungu.

Usiteseke kwa dhambi zako kisha ukasingizia msalaba wa Yesu Kristo, usiharibu mazingira ambayo Mungu amekuwekea toka uumbaji kisha ukaanza kumnung’unikia Mungu.

Ni kipindi hiki tunatakiwa kujihoji, na kujiuliza haya yanayotokea duniani ni mapenzi ya Mungu, au ni kazi ya yule mharibifu wa dunia? Roho Mtakatifu anapotufunulia hayo basi turejee haraka kwa Mola wetu.

Tunapotafakari haya yote ushiriki wetu katika ibada uwe wa unyenyekevu katika madhabahu ya Mungu.

Binadamu wamekuwa wakitesana wao kwa wao hivyo upendo wa Mungu umetoweka kabisa kwani ndugu kwa ndugu wanagombana na ugomvi hauishi.

Uonevu, unyanyasaji, udhalilishwaji na ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi imekuwa ndiyo desturi ya watu na wengi wanakuwa kama wanaochukia maendeleo, wanaharibu hata vitu vilivyowekwa kwa ajili yao.

Wengine wanadai mambo fulani fulani kwa faida yao, unaweza ukamkuta mtu anadai haki ya binadamu akakwambia sheria ya kuruhusu ushoga iwepo.

Huku ni kumkosea Mungu wetu, sheria ya Mungu iko ndani ya mioyo ya wanadamu, ni uasi tu unaochochewa na Ibilisi anayetaka tuangamie pamoja naye ndiyo unaowaka mioyoni mwetu.

Mungu ametupa amri kumi zinatushinda na hapo hapo tunataka atuongezee nyingine eti tutakuwa watiifu.

Mwanadamu fahamu kuwa Mungu ni mkuu, anao uweza wote, anayo mamlaka yote utukufu enzi na mamlaka ni vyake.

Vitu vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyake na kuna wakati ufikie tujiulize kwa nini hatubadiliki? Kuna matajiri wangapi wako Tanzania?

Hivi tajiri mmoja akiamua kuanzisha kiwanda cha bidhaa za hospitalini atakuwa ameokoa watu wangapi wanaokufa kwa magonjwa yanayotibika.

Kipindi hiki cha Kwaresima kituonyeshe njia ya kutoka katika utumwa wa kifikra, tukombolewe akili zetu zitumike kumtukuza Mungu na kanisa lake na kutoa huduma bora kwa jamii.

Watanzania wapatiwe mahitaji yao ya msingi ya kuwawezesha kuishi maisha yaliyo bora.

Kwa pamoja tuwe tayari kuzifanyia kazi rasilimali za nchi yetu ili ziweze kutumika kwa ajili ya manufaa ya wote.

Ninamshukuru sana Mungu kwa wewe msomaji wangu kwa kusoma mahubiri haya.

Mungu akubariki.



Chanzo: mwananchi.co.tz