Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahubiri ya Askofu Chengula yaliyotikisa

28320 Askofu+pic TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya, Evarist Chengula alifariki dunia  jana Jumatano Novemba 21, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Leo Alhamisi Novemba 22, 2018 Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima amelieleza Mwananchi kuwa Askofu Chengula atazikwa Novemba 27, 2018  jijini Mbeya.

Amesema ibada ya mazishi itafanyika Novemba 26 jijini Dar es Salaam na mwili wa marehemu kusafirishwa jijini Mbeya kwa ajili ya maziko.

“Tutafanya ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Novemba 26  katika ofisi za Baraza la Maaskofu Kurasini na baadaye tutaelekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kuelekea Mbeya kwa maziko,” amesema Dk Kitima.

Askofu Chengula atakumbwa kwa mengi, hasa ujumbe aliokuwa akiutoa kwa wananchi na waumini kuhusu masuala mbalimbali,  hasa uwajibikaji na kuhakikisha wanafanya mambo kwa ajili ya nchi yao.

Siku za hivi karibuni Askofu Chengula alitoa mahubiri yaliyotikisa.

Ilikuwa ni katika ibada ya Ijumaa Kuu Machi 30, 2018 Askofu huyo  aliwataka wakristo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa mwakani kwa kuchagua watu ambao hawatawafanya waishi kwa kuogopaogopa.

Ibada hiyo ilifanyika kitaifa katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatma, Mwanjelwa jijini Mbeya na kuonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC1).

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Chengula alisema ujumbe uliotolewa na maaskofu siku kadhaa zilizopita (mapema mwaka 2018) ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristo, lakini hawana imani ya dini hiyo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema.

“Tuangalie, kulialia tu hakuna maana. Tufikiri kabla ya utendaji kitu, sisi maaskofu tumeona udhaifu wetu ni huu, kila mara baada ya uchaguzi ndiyo tunaanza kum – analyse (kumchambua) mtu, kumtathmini mtu kwamba ataweza au hawezi.

“Hakuna maana tufurahie watu fulani tumewachagua, lakini tunaishi katika hali ya wogawoga, sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho,” alisema.

Aliwataka waumini kupitia jumuiya ndogondogo waanze kufikiria mwaka ujao watamchagua nani, “Mnielewe vizuri, si chama fulani, watu walio na tabia fulani. Tunataka nini, tunataka maendeleo, tunataka amani, tunataka watu tutendeane haki, lazima katika jumuiya ndogondogo tuwe tayari, tumeonyesha kifikra kwamba watu wa namna hii wapo katika jamii zetu.

“Pale watakapokuja kujiandikisha kwamba wanataka kupigiwa kura ya udiwani au uongozi wa vitongoji, tuwe tunajua kwamba tunamchagua mtu wa aina gani. Ujumbe wa mwaka huu tunasema hakuna maana kusikiliza kila kitu tu, badala yake tufikiri kabla ya kutenda.”

Askofu Chengula alifafanua kwamba kauli yake hiyo haimaanishi kwamba sasa ni wakati wa kuchagua chama fulani kwani wakifanya hivyo wataingia katika shimo lilelile, kwani watachagua mawazo ya watu fulani. “Je, wakiwapatia watu wasioendana na matarajio yenu mtasema nini?

“Tunafikiria yetu, tunataka chama fulani ndio kiongoze, ndio kitutendee sisi badala ya kufikiri waliochaguliwa wawe na lengo moja tu, kutufanya tupate haki zetu sisi Watanzania na kuishi kwa amani.”

Aliwataka waumini wajitathmini wao nani, wanataka mtu wa aina gani, “ili hata sisi tuweze kutimiza azimio la Umoja wa Mataifa walilofanya miaka 70 iliyopita kwamba lazima kila mmoja aishi akipatiwa haki akitendewa haki na mwisho kuwe na amani.”

“Wanangu sisi hatuna ubaya na mtu yeyote, ujumbe ule tumeutoa kwa kujiangalia wote, tuanze kujiandaa mwaka 2019 tuchague watu, tunaweza kukosea kwa sababu binadamu hana ukamilifu wa kufikiri, lakini kwa vyovyote vile hatutawatupia lawama watu wengine kwa sababu tumejitahidi kadri ya uwezo wetu...” alisema.

Alimtaka kila mmoja akitoka kanisani hapo aende akasimulie anakokwenda kwa sababu ni vita ya wote, kwa sababu wakipata viongozi wabaya wataumia wote na wakipata wazuri watafaidika wote na kila mmoja aone kiu kuona Tanzania yenye upendo.

“Kila anayekuja kubusu msalaba huu tulioulaza hapo mbele, amueleze Yesu nataka Tanzania yenye upendo,” alisema Askofu Chengula.

Soma zaidi:

Askofu Evarist Chengula afariki dunia

 



Chanzo: mwananchi.co.tz