Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli: Tutamkumbuka Askofu Chengula kwa kusimamia ukweli

28929 MAGUFULI+PIC TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameungana na waombolezaji wengine kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Evalisto Chengula.

Misa ya kumuaga Askofu Chengula aliyefariki Novemba 21, 2018 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu imefanyika leo Jumatatu Novemba 26, 2018 katika kanisa lililopo Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya misa hiyo Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa kanisa Katoliki kwa kuondokewa na kiongozi aliyekuwa akifanya vyema kazi yake ya kutangaza injili.

Rais Magufuli amesema pamoja na majukumu yake ya kutoa huduma za kiroho marehemu, Askofu Chengula alisimamia ukweli ikiwemo kupinga hadharani ndoa na mapenzi ya jinsia moja licha ya kuwepo mashinikizo mbalimbali.

Naye Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Flavian Kasalla amemshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano alioutoa wakati wa kuuguza na baada ya kifo cha Askofu Chengula.

Pia amewashukuru madaktari,  wauguzi, viongozi na wote waliokuwa wakimuombea kabla na baada ya kifo.

Waombolezaji wengine waliohudhuria misa hiyo ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna Mkapa, maaskofu, mapadre, watawa na waumini wa Kanisa Katoliki, ndugu jamaa pamoja na marafiki.

Mhashamu Askofu Chengula amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo na baada ya misa ya kumuaga mwili wake umesafirishwa kwenda Mbeya anakotarajiwa kuzikwa kesho Jumanne. 



Chanzo: mwananchi.co.tz